Rais Magufuli "Mjipendekeze Chato wakati nimeshaondoka kwenye Urais"
Rais John Magufuli ameelezwa kukerwa na kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kuomba feddha kiasi cha shilingi bilioni 1 za kujenga ofisi wilayani Chato mkoani Geita wakati tayari wana ofisi.
“Mmesema
hapa mnataka kujenga ofisi ya TAKUKURU wilayani Chato, lakini
tulishawapa jengo tena la ghorofa. Msizungumze mambo kwa kunifurahisha
mimi, mjipendekeze Chato wakati nimeshaondoka kwenye Urais,” ameeleza
Rais Magufuli.
Rais
Magufuli amesema hayo katika hafla ya kuzindua majengo saba ya taasisi
hiyo jijini Dodoma ambapo pia ameeleza kutoridhishwa na gharama
zilizotumika kuyajenga kwa sababu ni kubwa sana.
Amesema
kuwa tayari moyo wake umekuwa sugu hivyo hawezi kufurahishwa na mtu
anayezungumzia Chato kwa sababu yeye si mbinafsi. Akitilia mkazo katika
hilo ameiagiza taasisi hiyo kumchunguza mtumishi aliyependekeza ijengwe
ofisi nyingine Chato wakati tayari kuna ofisi na kwamba kitendo hicho
kinaweza kuwa na dalili za rushwa.
Mbali
na kuipongoza taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya kukabiliana na
rushwa nchini, lakini amesema ina mapungufu ikiwa ni pamoja na kushindwa
kuwachukulia hatua stahiki watumishi wake wanaotenda vitendo vya rushwa
pamoja na kuchelewesha kupeleka kesi za rushwa mahakamani.
Akizungumzia
gharama za nyumba hizo alizozizindua leo, amesema ni kubwa sana
ikilinganishwa na hali halisi ya nyumba zenyewe, lakini ameamua
kuzizindua kwa heshima kutokana na kazi kubwa ambayo TAKUKURU wamekuwa
wakifanya.
Katika
hatua nyingine ameahidi kutoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba za watumishi wa TAKUKURU jijini Dodoma, na ameagiza Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) lipewe tenda ya kujenga nyumba hizo mara baada ya
eneo la kujenga litakapopatikana.
Ameiasa
taasisi hiyo kuendelea kukabiliana na vitendo vya rushwa hasa kipindi
hiki cha uchaguzi mkuu ili kuhakikisha wananchi wanapata viongozi
wanaowataka na sio wale wanaotwaa madaraka kwa kutumia nguvu ya fedha
zao.
Post a Comment