HESLB yaanza kupokea maombi ya mikopo kwa 2020-2021, bajeti mwaka huu yaongezeka
Na Ismail Ngayonga - HESLB (0717 084252),
BODI
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumanne, Julai 21,
2020) imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa
mwaka wa masomo 2020/2021 kuanzia jana hadi Agosti 31, 2020.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi za HESLB zilizopo eneo la TAZARA jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema waombaji wote wa mkopo wanashauriwa kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa 2020-2021’ unaopatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).
“Mwombaji
anaweza kuingia kwenye mfumo wetu kupitia tovuti yetu ambayo ni
www.heslb.go.tz na atapata maelekezo ya kutosha ya kuingia katika mfumo
wa OLAS – Online Loan Application System,” amesema Badru.
Kuhusu
bajeti ya fedha za mikopo, Badru amesema Serikali imetenga TZS 464
bilioni kwa mwaka 2020/2021 ambazo zinatarajia kuwanufaisha jumla ya
wanafunzi 145,000. Kati yao 54,000, watakua ni mwaka wa kwanza na
wengine 91,000 ni wanaoendelea na masomo.
Bajeti ya mikopo kwa 2020-2021
“Bajeti
hii ya TZS 464 bilioni kwa 2020/2021 imeongezeka kutoka TZS 450 bilioni
mwaka 2019/2020 ambazo zinawanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119,”
amesema Badru wakati akifafanua swali la mwanahabari aliyetaka kujua
iwapo kuna ongezeko la bajeti.
Katika
mkutano huo, Badru pia amezungumzia wanafunzi wahitaji wa mkopo
waliomaliza kidato cha sita na wanatarajia kujiunga kambi za Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) na kusema utaratibu wa kuwafikia unaandaliwa.
“Tunafahamu
kuwa kuna wanafunzi waliomaliza kidato cha sita wanaotarajia kujiunga
na kambi 18 za Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia mwezi Agosti, 2020,
tunakamilisha utaratibu kwa kushauriana na Makao Makuu ya JKT ili
kuwawezesha kuwezeshwa wakati huo,” amesema.
Malipo ya robo ya nne ya fedha za chakula na malazi
Akitoa
ufafanuzi kuhusu malipo ya robo ya nne ya fedha za chakula na malazi
kwa wanafunzi waliopo vyuoni hivi sasa, Badru amesema HESLB inakamilisha
malipo hayo kwa wanafunzi 132,119 ambao wananufaika hivi sasa.
“Tumeanza
kulipa na tunakamilisha malipo hayo ambayo hulipwa kwa mwanafunzi
mnufaika moja kwa moja ili kumuwezesha kumudu gharama za chakula na
malazi katika siku zote anazokuwa chuoni kama tunavyoelezwa na chuo
husika,” amesema Badru na kuongeza:
“Ufafanuzi
huu tunautoa kwa kuwa tumepokea maoni kuwa baadhi ya wateja wetu ambao
ni wanafunzi hawajaelewa vizuri utaratibu huu wa malipo haya na ada za
mafunzo ambazo hulipwa mara mbili kwa mwaka,” amefafanua.
Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuomba
Akizungumza
katika mkutano huo, Afisa Mikopo Mwandamizi wa HESLB Josephat Bwathondi
amewakumbusha waombaji kuhakikisha wanafuata maelekezo ikiwemo kutumia
namba moja ya kidato cha nne katika kuomba mkopo na kuomba udahili
chuoni.
Kwa
mujibu wa Bwathondi, uzoefu wa uchambuzi wa maombi ya mikopo umeonesha
kuwa baadhi ya waombaji hukosea kwa kuambatisha nyaraka zisizotambulika
na hivyo kukosa mkopo na kushindwa kutimiza ndoto zao.
Post a Comment