RAIS DKT.MAGUFULI ARUDISHA FOMU YA MAOMBI YA KUOMBA RIDHAA YA KUTEULIWA MGOMBEA WA URAIS
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akionesha Fomu zake alizopata wadhamini mara baada ya kuzikabidhi kwa Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally Kakurwa katika Ukumbi wa NEC makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi pamoja na viongozi wengine wa Chama cha Mapinduzi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Philip Mangula, Katibu Mkuu Dkt. Bashiru Ally Kakurwa mara baada ya kuwasili katika Ukumbi wa NEC katika Makao Makuu ya CCM White House jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais John Magufuli, ambaye ni mgombea urais kupitia chama hicho amerudisha fomu za kugombea nafasi hiyo leo Juni 30, 2020, jijini Dodoma, katika ofisi kuu za chama hicho.
Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 17 mwezi huu Rais aliweza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kuwa Rais katika uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo Rais Magufu amevunja rekodi ya kupata kudhaminiwa na wanachama 1,023,911 Tanzania nzima.
“Nawashukuru sana Wenyeviti wa Mikoa yote mliamua ninyi wenyewe kwamba hizo fomu za wadhamini niwaletee ili mimi nisihangaike kuzunguka kila mahali, mmepata lawama watu wengi walitaka kudhamini lakini karatasi zikawa zimepungua ninaomba radhi sana kwa hilo”amesema Rais Magufuli
“Tarehe 17 mwezi uliopita niliamini kabisa kuwa, uchukuaji fomu wangu uwe kama kawaida yangu, nilijitahidi kuwatoroka vizuri sana, Katibu Mkuu akawa ananiuliza utakuja lini? Alipanga saa 5 mimi nikaja saa 2 nikachukua fomu nikaondoka.
“Najua changamoto za uongozi ni ngumu sana, zina mateso sana. Jana nimetoka Kilosa saa mbili, nimekuta mambo mezani, nimelala masaa matatu na nimelala peke yangu lakini kikubwa ni mimi nawashukuru sana.
“Niwaombe sana hasa wagombea wa CCM upande wa Zanzibar wawe waangalifu wasiumizane kwenye kunadi sera zao maana kazi sio urais tu. Hata kwenye majimbo watia nia mtarogana bure na kuumizana bure kwani atakayechaguliwa Mungu anamjua.
Nimeambiwa watia nia katika majimbo mengine wako zaidi ya 20, mtaragona, mtaumizana bure. Atakayechaguliwa ni mmoja tu. Kuanzia kesho tarehe moja mwenzi wa saba ruksa wana-CCM kupitapita ofisini kuchukua fomu kuomba ridhaa ya kuwania nafasi za uongozi.
”Tukigombana wakati wa kampeni tutapoteza mwelekeo hivyo atakayechaguliwa wakati wa kampeni tumbebe. Nafasi zipo nyingi za kuteua na hata sasa zipo kama nne sijateua. Najiuliza nimteue nani? Muhimu ni tushike dola kwanza.”
Kikao cha Kamati Kuu kitakaa Julai 10, 2020, ili kupitisha majina ya wagombea urais, Tanzania na Zanzibar.
Mkoa wa Morogoro umevunja rekodi kwa mikoa yote 32 kwa kumpatia udhamini mkubwa na wa kishindo ni wanachama 117,450,Geita wanachama 89,595,Mara wanachama 87,550,Dar es salaam wanachama 71,491,Tanga wanachama 62,839 hiyo ni baadhi ya mikoa iliyomdhamini Rais kwa idadi kubwa ya wanachama.
Jumuiya ya Umoja wa wanawake Tanzania, UWT wanachama 66,633 wamejitokeza pia kumdhamini Rais Dkt.Magufuli,Jumuiya ya Wazazi ya CCM wanachama 48,329 nao wamejitokeza kumdhamini Rais Dkt.Magufuli huku Jumuiya ya Vijana wanachama 103,063 nao wamejitokeza kumdhamini Rais Dkt.Magufuli
Katika hatua nyingine katibu Mkuu wa CCM Taifa Dkt.Bashiru Ally,amesema kuwa kuanzia kesho Tarehe Moja, nafasi za Ubunge na Udiwani zipo wazi. Wanachama wenye sifa kesho waanze kupita kwenye Ofisi kuulizia utaratibu.
Post a Comment