RAIS MAGUFULI : HALIIKIENDELEA HIVI TUTAFUNGUA VYUO NA MICHEZO
Serikali imesema kutokana na wagonjwa wa Corona kupungua katika vituo vilivyotengwa imepanga wiki inayoanza hali ikiendelea kuwa hivi kufungua vyuo ili wanafunzi nchini waendelee kusoma.
Kauli hiyo imetolewa leo mei 17, 2020 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa salamu katika kanisa la KKT Usharika wa Chato mkoani Geita.
Rais Magufuli amesema kuwa kwa taarifa za leo wagonjwa wamepungua, Amana ilikuwa ina watu 198 leo wamebaki 12 tu, Mlogonzila ilikuwa inalaza watu 30 leo wamebaki 6, kuna hospitali ilitengwa Kibaha kulikuwa na Wagonjwa 50 leo wamebaki watu 22 tena sio kwamba wamezidiwa.
Akizungumza Rais Magufuli amesema kuwa Arusha na Moshi wamebaki 11, vituo vingine havina wagonjwa, Mwanza wana vituo 10 lakini wamebaki 6 tu, Dodoma kuna vituo 4, kuna wagonjwa wawili, walikuwa wagonjwa 42 wengine wote wamerudi nyumbani.
Rais Magufuli amesema kuwa pia Idadi imezidi kupungua katika Hospitali za Agakhan wamebaki 31, Hindulmandal 16, Regency 17, TMJ saba na Rabininsia 14.
Aidha katika hatua nyingine Rais Magufuli amesema kuwa kuna mashirika ya ndege tayari yameshasajili watalii, wengine mpaka mwezi wa 8 ndege zimejaa, kwa ajili ya kuja Tanzania kutalii, nimeiagiza wizara husika kuziruhusu ndege hizo ziingie nchini na wala hawatowekwa siku 14 za uangalizi.
“Tanzania ni taifa huru na linalojiamini, ni taifa ambalo limepambana na majanga mengi hivyo nataka niwahakikishie uchumi wetu unaenda vizuri, endeleeni kuchapa kazi kwa sababu Tanzania hakuna ‘lockdown’”,ameeleza Rais Magufuli.
“Sisi ni taifa huru hatuwezi kukubali Corona itutawale. Uchumi wetu ni namba moja tukiufanya uchumi wetu ukalala hata mishahara wala sadaka tusingeweza kutoa, maisha lazima yaendelee”, amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa kuongezea Rais Magufuli amesema kuwa katika kupambana na ugonjwa huu vipo vingi vimejitokeza, natoa wito kwa Wizara ya Afya na madaktari nchini kuwa mtu anapofariki kwa ugonjwa wowote hata kama ni Corona azikwe kiheshima kama ilivyokuwa kawaida.
Rais Magufuli ameendelea kusema Corona sio Ebola, mbona wenye UKIMWI, TB au Surua hatuwafanyii hivyo wakati vyote hivyo ni virusi! Mwelekeo huu ni wa hovyo. Ugonjwa huu utasambaa lakini baadae utaisha.
“ Sikufunga mipaka maana ukifunga kuna nchi tutazinyima uchumi wao na kudumaza uchumi wa watu wanaozalisha vitu vinavyotakiwa kupelekwa nchi nyingine, tulikua tuna uhaba wa sukari tani 40,000, tungefunga mipaka sukari tungeipataje?” ameuliza Rais Mgufuli.
Rai Magufuli mametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchapa kazi hasa kwa wakati huu ambao mvua ziko mwishoni, tuendelee kulima mazao madogo madogo yanayoweza kuhimili mvua kidogo.
Post a Comment