Ads

Rais Magufuli atoa maagizo kwa wakuu wa mikoa inayopakana na Kenya


Rais Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa mitano nchini ambayo iko katika maeneo ya mpaka wa Tanzania na Kenya pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele kukutana na wenzao wa Kenya ili kutatua mgogoro ambao umeonekana kujitokeza katika siku za hivi karibuni.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa mkoa wa Singida na kuongeza kuwa mgogoro huo ambao umejitokeza katika maeneo ya mipakani baada ya madereva kuzuiwa kuingia katika nchi hizo kutokana na hofu ya maambukizi ya corona ni lazima umalizwe.

Amesisitiza kuwa Tanzania na Kenya ni marafiki na ndugu, hivyo virusi vya corona haviwezi kudhoofisha urafiki huo.

Rais Magufuli amesema yeye pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wameishamaliza jambo hilo na kwamba anataka mgogoro huo umalizike kabisa hata kwa viongozi wa ngazi ya chini.

“Juzi nilipigiwa simu na Kenyatta nikiwa bado Chato, akanipa pole na kujielezea mambo ya corona kidogo, leo pia mimezungumza nae pia, kuna kimgogoro kule mpakani mwa Kenya, Kenya ni Marafiki zetu, corona isiwe chanzo cha migogoro, sisi Marais tumeyamaliza

“Viongozi wa Mikoa wasitatue matatizo kwa jazba, nafahamu ukichokozwa sana ukanyamaza na wewe unachokoza kidogo sio mbaya, ila tumeyazungumza na Kenyatta tumeyamaliza, Mawaziri na Wakuu wa Mikoa pia mkutane na wenzenu Kenya yaishe haya, ndani ya wiki hii “- Amesema Rais Magufuli

Hivi karibuni madereva wa magari kutoka nchini Tanzania walizuiliwa kuingia nchini Kenya, hali iliyosababisha mamlaka kwa upande wa Tanzania nazo kuwazuia baadhi ya madereva wa magari kutoka Kenya kuingia nchini.

No comments