Meya Manispaa Morogoro aanza ziara ya kikazi na Choo cha Mtoto wa Kike.
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, ameanza ziara zake za kikazi za kukagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Morogoro ambapo ameanza kutembelea ujenzi wa Choo cha mfano cha mtoto wakike kilichojengwa Shule ya Sekondari Tubuyu Kata ya Tungi.
Ziara hiyo ameianza leo Mei 15, 2020 kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa Choo cha Mtoto wa kike pamoja na Stendi ya Mabasi Msamvu kwa ajili ya kuangalia hali ya ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Kihanga, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, kwa usimamizi mzuri na maono ya kipekee ya kutekeleza kwa haraka na wepesi maagizo ambayo yaliadhimiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutaka vyoo hivyo vijengwe.
Aidha , amesema kuwa uwepo wa choo cha maalum cha mtoto wa kike kitamwezesha kukaa shuleni kwa muda mrefu kushiriki masomo kikamilifu badala ya kubaki nyumbani wakati wa hedhi hali inayoathiri mtiririko wa maudhurio darasani.
“"Wanafunzi wa kike wanakabiriwa na changamoto mbalimbali , lakini kama mnavyofahamu tatizo la vyoo katika shule zetu ni kubwa sana kwani watoto ni wengi na matundu ya vyoo ni machache, nampongeza sana Mkurugenzi kwa kuliona hili, lakini pia nampongeza na Mkuu wa Shule kwa usimamizi mzuri bila kuwasahau wahandisi wetu wa Manispaa kwa kutujengea choo cha mfano ndani ya Mnaispaa yetu na Mkoa kwa ujumla, hivyo nitoe wito kwa wadau wengine waliopo ndani ya Manispaa yetu kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ili watoto wetu wajisitiri katika vyoo safi na salama ambavyo vitakuwa rafiki kwa watoto wa kike Shuleni ” Amesema Kihanga.
“ Tunatakiwa kukitunza hiki ni choo cha mfano, hatujajua wenzetu wamejenga vyoo vya aina gani lakini nina uhakika tukipata wageni tutawaleta hapa kuja kujifunza, sitarajii tunawaleta wageni harafu choo mmeshaanza kukiharibu, kitunzeni vizuri hiki ni choo cha mfano, nitawaleta Waheshimiwa Madiwani kutembelea na kuona kitu kinachofanyika hapa “ Ameongeza Kihanga.
Kihanga amesema kutokana na tafiti zilizofanyika kuhusu sababu zinazochangia mahudhurio hafifu ya mtoto wa kike darasani ni kutokana na mabadiliko ya maumbile wanapoingia ambapo kuna mifumo ya vyoo visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana wanaoingia hedhi huleta changamoto kubwa kwao.
Hata hivyo ,amesema Shule za Sekondari zipo nyingi sana na hawana fedha za kutosha lakini amemuomba Mkurugenzi katika awamu ijayo katika bajeti ya 2021/2022 waweze kutenga fedha ili waongeze angalau vyoo vyengine ili wasiwe na matabaka tofauti tofauti .
Katika hatua nyengine, amewataka waalimu kuendelea kutoa elimu bora kwani mazingira mazuri ya shule yanaendana na matokeo mazuri.
Amesema sifa ya Mwalimu ni kufaulisha vizuri , hivyohivyo kwa wazazi pia ni kuona watoto wao wamefaulu.
Amemtaka Mkuu wa Shule kusimamia kikamilifu choo hicho mara baada ya kukabidhiwa kwani imekuwa ni desturi kwa jamii nyingi kitu kinavyoanza kuwa kipya baada ya miezi miwili uharibifu unafanyika.
Wakati huo huo amesema ubora wa vyoo vya watoto wa kike uendane na vyoo vya wanaume ili kuepeuka kutengeneza Taifa lenye matabaka mawili.
Amesema choo hicho mara baada ya kukamilika kitakuwa na matundu maalumu kwa ajili kuwafikia watoto wa kike wenye ulemavu.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Tubuyu, John Kamunu Mniko, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kujali wanafunzi wa kike kwa kuwajengea choo cha mfano cha mototo wa kike.
“ Tunampongeza Mkurugenzi wetu wa Manispaa kwa kweli ametupa heshima sana, tunatambua katika Manispaa yetu shule zipo nyingi lakini choo hiki kimekuja kujengwa kwetu, tunashukuru ushirikianao tunaoupata kutoka kwa Afisa elimu wetu, wahandisi wa Manispaa, na Meya kama hivi umekuja tumefarijika sana tukuhakikishie tu mara baada ya ujenzi huu kukamilika tunaenda kuongeza angalau ujenzi wa matundu vyoo vya walimu kwakuwa tumejipanga na haya maligahafi yatakayobakia katika ujenzi huu tutayatumia,” Amesema Mwl Mniko.
Choo hicho kimejengwa kwa thamani ya Shilingi Milioni 35 ambapo kinajumuisha matundu 12, matundu 2 ya walemavu, bafu na sehemu ya kuvalia nguo na kujiangalia baada ya kumaliza haja zao.
Post a Comment