Ads

TAKUKURU MANYARA YAWASHIKILIA MAWAKALA WATATU

Mkuu wa Takukuru Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
…………………………………………………………………………………………
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani Manyara, inawashikilia mawakala watatu wa ushuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kudaiwa kupokea rushwa.
Mkuu wa Takukuru wa mkoa wa Manyara, Holle Makungu akizungumza jana alisema mawakala hao walikamatwa juzi wakiwa wanajipongeza kwa kunywa vinywaji kwenye bar ya Mandosi iliyopo Dareda kati.
Makungu aliwataja mawakala hao kuwa ni Idd Sulle na Ezekiel Samwel wa kituo cha kazi cha kizuizi cha Kampala na Basil Aloyce wa kizuizi cha Sinai.
Alisema mawakala hao wanadaiwa kuomba na kupokea rushwa ya sh120,000 ili kutoa kibali cha kusafirisha mazao yao kutoka mkoani Singida kwenda jijini Arusha.
Alisema mawakala hao wa kituo cha Kampala walimsimamisha mfanyabiashara huyo akiwa na mazao yake kituo cha Sinai mjini Babati na kuchukua nyaraka zake.
“Mfanyabiashara huyo alikuwa na mazao ya mchele, vitunguu na viazi mviringo akisafrisha kwenda kuuza jijini Arusha, alitii agizo hilo kisha kesho yake akafuata nyaraka zake,” alisema Makungu.
Alisema baada ya kufuata nyaraka hizo aliambiwa awapatie rushwa ya sh120,000 ili watie saini nyaraka hizo na yeye aendelee na safari yake akiwa na mazao hayo ndipo akatoa taarifa Takukuru nasi tukaweka mtego.
“Ukiacha kucheleweshwa kwa sababu za rushwa kwa mfanyabiashara huyo, baadhi ya mazao kama vitunguu na viazi vimeharibika hivyo watuhumiwa pamoja na kufikishwa mahakamani watawajibika kwa kulipia hasara hiyo,” alisema.
Alitoa rai kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Manyara, kuweka mawakala waadilifu kwenye vizuizi ili kuondoa usumbufu na kudhibiti upotevu wa mapato unaofanywa na mawakala wasio waadilifu.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Babati, walidai kuwa tatizo hilo ni la muda mrefu kwani baadhi ya mawakala wanakusanya ushuru wamekuwa wakipata rushwa kwa kutumia mtindo huo.
Mfanyabiashara wa mazao Elias Umbu alisema mawakala hao wanapaswa kubadilika na kutambua kuwa nyakati za kuchukua rushwa kwenye mazao zimepita waridhike na wanachokipata.

No comments