Ads

NEC YAKUTANA NA VIONGOZI VYAMA VYA SIASA KUJADILI MABORESHO DAFTARI LA WAPIGA KURA

KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2020 Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imekutana na viongozi wa vyama vya siasa na kutoa taarifa ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya pili.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa NEC Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage alisema uwekaji wazi daftari la Awali utafanyika sambamba na Uboreshaji wa  Daftari la Awamu ya Pili na kusisitiza zoezi la uboreshaji litaanza Aprili 17 na kukamilika Mei 4 mwaka huu.
“ Mazoezi ya uwekaji wazi Daftari la Awali na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura yatafanyika kwa siku tatu tu kwenye kila mkoa na katika route mbili baada ya route ya tatu zilizopangwa hapo awali,” alisema Jaji Mstaafu Kaijage.
Alibainisha kuwa mazoezi hayo yatafanyika Aprili 17 hadi 19 mwaka huu na kwamba jumla ya  mikoa 12 na vituo vya uandikishaji 2005 vitahusika huku akikazia route ya kwanza itahusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora.
Alisisitiza kuwa upande wa route ya pili mazoezi hayo yatafanyika kuanzia Mei 2 hadi 4 mwaka huu Zanzibar na mikoa 14 ya Tanzania Bara ambapo vituo vya kuandikisha wapiga  2001 vitahusika na kubainisha  mikoa itakayofikiwa katika route ya pili ni Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi , Mtwara, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa  jumla ya vituo vya  kuandikisha Wapiga kura vitakavyotumika katika awamu hii ni 4,006 badala ya vile 8,031 vilivyotajawa awali na kwamba kati 3,956 vitakuwa Tanzania Bara na 50 vitakuwa Tanzania Zanzibar.
Jaji Mstaafu Kaijage alisema uboreshaji utafanyika katika kila kata  ambapo kutakuwa na Mwandishi Msaidizi na BVR Kit Operator ambao watakuwa  na orodha ya vituo vyote vya kata husika  na kubainisha watendaji hao watakuwa na uwezo  kuboresha taarifa za mpiga kura yeyote atakayefika kituoni kulingana na kituo atakachopigia kura siku ya uchaguzi.
Katika hatua nyingine alisema tayari NEC imenunua vifaa kwa ajili ya kuchukua tahadhari za Ugonjwa wa COVID- 19 unaosababishwa na Virusi vya Corona pamoja na kutoa maelekezo kwa watendaji wa uboreshaji kuzingatia miongozo ya afya.
Aliwasisitiza wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura mwaka 2015 na wale wa Daftari la waliomo kwenye Daftari la Awamu ya Kwanza kujitokeza kwa wingi kuhakiki taarifa wakati daftari litakapowekwa wazi kwenye maeneo yao.
Aidha, alisema wananchi wenye sifa ya kujiandikisha kufika vituoni mapema zoezi litakapowafikia na kwamba wasisubiri kujitokeza siku za mwisho wa zoezi ili kupunguza msongamano katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona.
NEC  imeeleza kuwa njia za kuhakiki taarifa za wapiga kura ni kufika vituoni walivyojiandikisha, mpiga kura kupiga namba *152*00# na  kupitia tovuti www.nec.go.tz

No comments