Ads

NAIBU WAZIRI MABULA ACHOSHWA NA BAJETI ZA UPIMAJI ARDHI HALMASHAURI ZA MKOA WA KAGERA


Na Munir Shemweta, WANMM KAGERA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameonesha kutoridhishwa na kiasi cha fedha kilichotengwa na halmashauri nane za mkoa wa Kagera kwa ajili ya shughuli za kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo ya halmashauri hizo.

Hali hiyo inafuatia Naibu Waziri Mabula kuwahoji wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Kagera kutaka kujua kila halmashauri ya mkoa huo imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya shughuli za upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi katika bajeti ijayo ya mwaka 2020/2021 ikiwa ni juhudi za kuhakikisha maeneo yote yanapimwa ili kuondoa migogoro ya ardhi na kuongeza mapato kupitia sekta ya rdhi.

Akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Kagera jana Dkt Mabula alibaini halmashauri mbili za Misenyi na Kyerwa katika mkoa wa Kagera ndizo angalau zilizoonekana kutenga shilingi milioni 30 kwa kila moja kwa ajili ya shughuli za upangaji na upimaji ardhi katika maeneo yao.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa halmashauri ya Misenyi  Innecent Mkandara halmashauri yake imetenga milioni  50 kwa ajili ya shughuli za ardhi na milioni 30 kati ya hizo zitatumika kwa kazi ya upimaji huku mkurugenzi wa Kyerwa Shadrack Magamba akieleza halmashauri yake kutenga milioni 30 kwa kazi za upimaji sambamba na milioni 25 kwa ajili ya upimaji vijiji.

Halmashauri nyingine za mkoa huo zimetenga chini ya milioni 30 huku halmashauri ya Karagwe ikiwa ya mwisho kwa kutenga milioni 13 huku Mkurugenzi wake Godwin Kitonga akieleza kuwa sehemu kubwa ya halmashauri inayofanyika shughuli ya urasimishaji.

Dkt Mabula alisema kiasi kilichotengwa na halmashauri za mkoa wa Kagera katika kazi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi ni kidogo sana na hakioneshi kama wakurugenzi wake wana nia ya dhati ya kupima maeneo yao kwa kasi inayotarajiwa na wizara wakati halmashauri hizo ndizo zenye mamlaka ya upangaji kwenye maeneo yake.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi alisema katika kuhakikisha maeneo yote yanapangwa na kupimwa tayari wizara imeanzisha utaratibu wa kuzikopesha halmashauri fedha isiyo na riba kwa ajili ya shughuli za kupanga, kupima na kumilikisha maeneo ambapo kwa mwaka huu wa fedha  unaoisha halmashauri 24 zilikopeshwa na nne kati ya hizo ndizo zilizofanikiwa kurejesha mkopo huo kwa asilimia mia moja.

‘’Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara ya Ardhi inatarajia kupatiwa bilioni saba kwa ajili ya kuzikopesha halmashauri, ni vizuri wakurugenzi mkatumia fursa hiyo kwa kuandika andiko litakalowawezesha kupata mkopo huo kulingana na maombi’’ alisema Dkt Mabula.

Sambamba hilo, aliwataka wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Kagera kuhakikisha maeneo yote ya umma yanapimwa kufikia mwezi julai mwaka huu na kupatiwa hati ili kuondoa changamoto ya kuvamiwa na kupunguza migogoro ya ardhi ianyosababishwa na mipaka.

Akigeukia suala la mapato yatokanayo ya kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula alisema mkoa wa Kagera unaweza kuwa mkoa wa mwisho na kufuatiwa na ule wa Rukwa kwa kukusanya mapato kidogo ya sekta ya ardhi. Hali hiyo inafuatia kuelezwa kuwa hadi sasa mkoa huo umekusanya shilingi milioni 801 kati ya bilioni 3.3 ilizotakiwa kukusanya ambazo ni sawa na asilimia 23.

‘’Kwa mtindo huu hatuwezi kufika, tukisimamia vizuri sekta hii kwa kukusanya kodi ya ardhi tutamsaidia mhe rais kusimamia miradi ya kimkakati ambayo mingi inaendeshwa kwa fedha za ndani na sekta ya ardhi ikisimamiwa vizuri inaweza kukusanya fedha kuliko sekta nyingine’’ alisema Mabula.

No comments