Cti kufanya Mkutano wa Majadiliano na Waziri Kairuki Dar.
Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (Cti) limesema linatarajia kufanya Mkutano wa Majadiliano na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki Machi 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho hilo Leodgar Tenga alisema sababu ya msingi ya kukutana na waziri huyo ni kujadiliana masuala muhimu ya sekta ya viwanda hasa wakati nchi ikielekea uchumi wa kati kupitia sekta hiyo.
“ Tumedhamiria kukutana na kukutana na kiongozi huyo tukiamimi Cti na wanachama wake watapata fursa ya kujadili na kutoa mapendekezo yatakayoisukuma sekta ya viwanda kufikia uchumi wa kati,” alisema Tenga.
Alibainisha kuwa wanachama wa Cti watapata nafasi ya kubadilishana mawazo yatayoisaidia sekta ya kupiga hatua pamoja kueleza changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Alisisitiza kuwa wana Cti watapata fursa ya kujadili yaliyomo na yalipofikia Mapendekezo ya kusaidia kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint) na kuwasisitiza wasio na wanachama kuhudhuria mkutano huo.
Alifafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya makubwa katika kuhakikisha sekta hiyo inachochea uchumi wa kati ikiwemo Ujenzi wa Reli ya Kisasa, Bwawa wa Stiglers Gorge, uboreshaji wa bandari pamoja na barabara.
Pia alisema serikali katika kuhakikisha inaboresha mazingira ya biashara imefanya mambo mbalimbali ikiwemo ufutaji wa tozo 54 kwa wafanyabiashara na kwamba bado wanaendelea kushirikiana nayo lengo likiwa kuboresha uwekezaji kwenye viwanda.
Alitoa wito kwa watanzania kuchukua tahadhari ya kupambana na ugonjwa hatari wa Homa kali ya Mafua (Corona) kwani ugonjwa huo una madhara kwenye sekta ya viwanda huku akikazia maendeleo ya viwanda hutegemea watu wenye afya.

Post a Comment