WAZIRI MKUU AAGIZA WADAIWA WOTE NHC WALIPE MADENI KABLA YA MEI 30
Mwambawahabari
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameuagiza uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC) uwaandikie barua wapangaji wote wanaodaiwa kodi na shirika hilo na
wahakikishe zimelipwa ifikapo Mei 30, mwaka huu.
“Orodha ya wadaiwa
niliyonayo hapa ni kubwa na wengine inaonesha wamehama na wameondoka bila
kumalizia kodi zao. Hawa wote ni lazima tuwafuatilie na walipe madeni yao,”
amesema.
Ametoa agizo hilo
leo (Jumanne, Februari 11,
2020) wakati akizungumza na viongozi na wajumbe wa Bodi
ya shirika hilo kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar
es Salaam.
“Taasisi zote
za Serikali ambazo zimepanga kwenye nyumba za shirika ni lazima zilipe madeni.
Chombo chochote cha Serikali kinaishi na bajeti, kwa hiyo hata kama wamejenga ya
kwao, walipaswa walipe kabla hajahama.”
“Waandikieni
barua wadaiwa wote ili walipe. Tunaelekea mwishoni mwa bajeti ya mwaka huu, na
hawa wote wawe wamelipa ifikapo tarehe 30 Mei, 2020. Nami nipate orodha ya taasisi
za Serikali zinazodaiwa ili niwafuatilie; nitawaita Makatibu Wakuu wao mmojammoja.
Hao wadaiwa binafsi wachukulieni hatua stahiki,” amesisitiza.
Waziri Mkuu
amesema madeni ambayo taasisi za Serikali zinadaiwa yanafikia sh. bilioni 4.3
na kama zitalipwa zote hizo, zitalisaidia shirika kuendelea na mpango wake wa
ujenzi wa nyumba nafuu kwenye maeneo mbalimbali.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amelitaka
shirika hilo lijielekeze kwenye ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu kwa
sababu mahitaji ya nyumba nchini bado ni makubwa. “Simamieni suala hili, ili tupate
nyumba nzuri na za bei nafuu. Simamieni wataalamu wenu ili wasikadirie miradi
ambayo bei zake zitakuwa juu sana na kisha wananchi wetu washindwe kumudu. Ni
lazima mhakikishe kuwa wananchi wa kipato cha chini wananufaika na uwepo wa
shirika,” amesema.
Amesema
wataalamu hao wanahitaji kudhibitiwa kwa sababu sehemu kubwa ya malighafi inapatikana
hapa nchini. “Hivi sasa kokoto, nondo, mabati na vifaa vingi vya ujenzi
vinazalishwa hapa nchini, siyo kama zamani. Iweje bei ya kuuza nyumba inakuwa
ya kutisha?” alihoji.
Pia Waziri
Mkuu aliwataka viongozi hao waimarishe ukusanyaji wa mapato ya shirika hilo kwa
kuhakikisha kodi zinakusanywa kwa njia ya kielektroniki. “Tuache tabia ya
kuruhusu maafisa kwenda nyumba kwa nyumba na kudai shilingi 500,000 kwa risiti
za kuandika. Tumieni control number,
ili mwananchi aweze kulipia kwa simu au benki na hela inaingia moja kwa moja
katika shirika,” amesema.
Mapema, akitoa
taarifa ya shirika hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Sophia
Kongele alisema shirika hilo linawadai wapangaji waliohama na waliopo ambao wengi
wao ni wizara na taasisi za Serikali na akaomba wahimizwe kulipa ili wao waweze
kuendesha shirika kwa ufanisi.
“Kwa
wapangaji waliohama bila kulipa, shirika linadai shilingi bilioni 4.353 na kwa
wapangaji waliopo wanadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.286, na hivyo kufanya
deni lote lifikie shilingi bilioni 5.641.”
Alisema shirika
hilo limekuwa likiendesha miradi ya ndani na ya nje ikiwemo kutekeleza miradi
ya ujenzi ya taasisi nyingine kama mkandarasi na mshauri. “Shirika limefanikiwa
kumaliza miradi 16 ya ukandarasi yenye thamani ya shilingi bilioni 16.8 na
linaendelea na ujenzi wa miradi 10 ya ukadarasi yenye thamani ya shilingi
bilioni 69.4,” alisema.
Alisema
wanaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya Morocco
Square, Seven Eleven (Kawe), Golden Premier Residence (Kawe) na Regent Estate
ambayo kwa sasa imesimama kutokana na ukosefiu wa fedha.
Post a Comment