Ads

MWAKALINGA AKABIDHI VIFAA VYA MAFUNZO CHUO CHA UJENZI MOROGORO.

Mwambawahabari

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, amekabidhi mtambo mmoja (Grader) na Komyuta 20 kwa Uongozi wa Chuo cha Ujenzi Morogoro na kutoa wito kwa wazazi, walezi, wafadhili na waajiri wote kuwapeleka vijana na watumishi wa jinsia zote  kupata mafunzo ya ufundi stadi ili kuweka uwiano mzuri kati yao.
Wito huo ameutoa mkoani Morogoro akiwa kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambapo pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu huyo amesema kuwa hafurahishwi na kuwepo kwa idadi ndogo ya wanawake katika baadhi ya kozi, Chuoni hapo.
"Nimesikitika kupata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Chuo kuwa kozi nyingi zina idadi kubwa ya wanaume kuliko wanawake na nyingine zina wanaume pekee, elimu ya ufundi stadi ni kwa wote, shime jinsia zote kushiriki kupata mafunzo haya", amesema Mwakalinga.
Katibu Mkuu Mwakalinga, amefafanua kuwa utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana utatoa mchango mkubwa katika azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ambapo fani za ujenzi ni muhimu katika kufikia azma hiyo.
Aidha, Mwakalinga ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kwa kukubali kutoa mtambo mmoja (Grader) na Wizara kutoa kompyuta 20 ili vitumike kufundishia wanafunzi ambapo amesema kuwa vifaa hivyo vitakuwa chachu ya utoaji mafunzo hapo chuoni.
"Naamini sasa kuja kwa vifaa hivi kutarahisisha na kuhamasisha mafunzo kwa vitendo, nawasihi mtumie vifaa hivi kwa malengo yaliyowekwa pamoja na kuvitunza vizuri", amesisitiza Katibu Mkuu Mwakalinga.
Sambamba na hilo Katibu Mkuu Mwakalinga amesema kuwa Wizara ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha Taasisi ya Teknolojia yaUjenzi kwa kuunganisha Chuo cha Ujenzi Morogoro na Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi kilichopo Mbeya ambapo amefafanua kuwa lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni kuboresha mafunzo yanayotolewa na vyuo hivyo viwili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Morogoro, Melkizedeck Mlyapatali amesema kuwa chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi wakiwemo wahandisi wa fani mbalimbali, wakufunzi, wahasibu na wafanyakazi wengine kutokana na wafanyakazi wengi kustaafu kwa mujibu wa sharia na wengine kufariki dunia.
Chuo kina jumla ya wanafunzi 403 na kinaendesha mafunzo ya ufundi stadi na masomo ya kawaida kwa lengo la kuwezesha wahitimu kuwa mahiri katika Nyanja za ujenzi.

1 comment:

  1. I need to know, which qualification is required to join chuo Cha ujenzi morogoro?

    ReplyDelete