Ads

Moto Kichaa Watia Hasara Wilayani Njombe


NJOMBE
Licha ya halmashauri ya wilaya ya Njombe kutegemea mapato yake kutoka kwenye sekta ya misitu kwa asilimia 75 lakini ongezeko la matukio ya moto kichaa katika maeneo mengi ya wilaya hiyo yatokanayo na shughuli za kibinadamu yameendelea kuwa tishio kwa muda mrefu katika  sekta hiyo.
Takwimu zinaonyesha takribani asilimia 70 ya miti inayopandwa nchini imekuwa ikifa kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukame,moto na nyinginezo za binadamu jambo ambalo limeisukuma serikali kuanza kutoa elimu kwa umma juu ya malezi na matunzo ya miti  kwa manufaa ya baadae.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika shamba la kikundi cha ujasiriamali cha JUPAHIMA katika kijiji cha Matiganjora wilayani Njombe mkuu wa wilaya hiyo Ruth Msafiri ameonyesha kutofurahishwa na takwimu hizo na kuagiza serikali zote za vijiji kutunga sheria kali dhidi ya wanaosababisha mioto kicha huku pia akitaka sheria hiyo kuwa na kifungu ambacho kinaitaka kila kaya kuwa na ekari moja ya miti ili kuwa walinzi .
Katika hatua nyingine Msafiri amefungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza viwanda vya kuongeza thamani malighafi za misitu wilayani kwake ili kuepukana na biashara ya mazoea ya kuuza miti ya mbao na boriti.
Awali mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Hamad Maguo akifafanua jitihada zinazochukuliwa katika kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali kuwekeza katika sekta ya kilimo anasema vikundi 31 vimepatiwa elimu pamoja na kuanzisha mashamba darasa 26 huku wakala wa misitu Tanzania TFS wakiendelea kutoa usaidizi wa kifedha na elimu kama ambavyo Audatus Kashamakula anavyoeleza.
Baadhi ya wanakikundi cha JUPAIMA akiwemo Jaktan Mwani ambaye ni mwenyekiti wa kikundi na Yudith Mhoka wanaeleza faida wanayoipata kwa kuwekeza katika miti na nyuki.
Takribani miti 2500 imepandwa kwa ufadhili wa TFS katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti wilaya ya Njombe uliofanyika katika kijiji cha Matiganjola kata ya Ikuna.

No comments