WAZIRI LUKUVI AWAPA KIBARUA WAKUU WA MIKOA
NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ametoa wito kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha wanawalinda wamiliki wa ardhi ambao wapo kisheria.
Waziri Lukuvi alitoa agizo hilo jana Desemba 05, 2019 wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji uliofanyika mjini Kibaha na kuongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki.
wawekezaji na wafanyabiashara walipata nafasi kufikisha malalamiko yao ambayo ni kikwazo katika shughuli zao.
Waziri Lukuvi alibainisha kuwa Mkoa wa Pwani unaongoza kwa uvamizi ambapo Wilaya ya Bagamoyo inatajwa kuwa kinara.
Lukuvi alisema, wakuu hao wa mikoa wana askari wanaweza kuwaondoa waliojimilikisha ardhi kinyume cha sheria.
“Tumieni mabaraza ya ardhi yaliyoundwa kisheria kuondoa wavamizi kwenye maeneo ambayo yanamilikiwa kisheria" alisema.
Naye Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga aliwahimiza wawekezaji kuwekeza kwenye kilimo cha alizeti na michikichi kwa ajili ya mafuta ya kupikia.
Waziri Hasunga alisema, kuna uhitaji wa mafuta ya kula tani 650 ambazo kiasi cha shilingi billion 675 zimekuwa zikitumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.
Alisema, upande wa mafuta wawekezaji ni wachache, hivyo wakipatikana wawekezaji wengi wataokoa fedha ambazo zinaenda nje ya nchi zibaki hapa nchini.
Aidha kuhusiana na mikopo kwa wakulima alisema, kwa anayetaka kulima awasiliane na mfuko wa pembejeo pamoja na benki ya kilimo kupata taratibu.
Akihitimisha mkutano huo Waziri Kairuki amewahahakikishia kuwa majibu yote ambayo hayajapatikana papo hapo wizara inaandaa bango kitita ambalo malalamiko na changamoto zote zitajumuishwa na kupelekwa ngazi zote akiwemo Mhe. Rais na Waziri Mkuu.
Amewapongeza wawekezaji wazao ambao wameweza kusajili miradi zaidi ya 70 kwa mwaka huu pekee huku akizitaka taasisi za kibenki kuondoa urasimu katika kutoa mikopo kwa wawekezaji wazawa badala yake waweke mazingira rafiki.
Mkutano huo wa mashauriano wa siku moja ulihudhuriwa na mawaziri watatu pamoja na manaibu Mawaziri tisa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi , Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Sima, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Constantine Kanyasu ,Naibu Waziri wa Mambo wa Ndani ya Nchi,Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde (Kazi, Vijana na Ajira), Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Josephat Kandege.
Pia ulihudhuriwa na Taasisi wezeshi, mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, mwenyekiti wa wafanyabiashara ndogondogo machinga, wawekezaji pamoja na viongozi wengine kutoka Halmashauri na Mkoa.
Post a Comment