RC MAKONDA APIGA MARUFUKU KAMPUNI YA NYANZA KUPEWA KANDARASI DAR.
Mwambawahabari
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo Novemba 02 amewataka TANROAD kuhakikisha Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza haipatiwi mradi wowote wa ujenzi ndani ya mkoa huo baada ya kampuni hiyo kuendelea kusuasua kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Kivule licha ya Kupewa fedha za ujenzi.
RC Makonda ametoa onyo hilo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambapo akiwa kwenye barabara ya Kivule ameshuhudia Mkandarasi huyo akiwa na uhaba wa Vifaa licha ya kudanganya kwenye mikataba kuwa anavyo vifaa vya kutosha ili apatiwe tenda.
Aidha RC Makonda amezionya bodi za manunuzi zinazotoa tenda Kwa kuendekeza Rushwa na kujuana jambo linalowafanya kushindwa kumuonya mkandarasi kwakuwa tayari wamefungwa midomo Kwa rushwa.
Katika ziara hiyo RC Makonda ametembelea ujenzi wa Machinjio mpya ya Vingunguti ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo ambao kwa sasa upo kwenye hatua ya kufunika gorofa ya kwanza huku akieleza kuwa anaamini ujenzi utakabidhiwa Mwezi Disemba.
Katika hatua nyingine RC Makonda ametembelea ujenzi wa Mto Sinza na Mto Ng'ombe wenye urefu wa Km 7.5 ambao baada ya kuwakamata wakandarasi hatimae ujenzi sasa umeanza huku akimtaka mkandarasi wa kampuni hiyo kumaliza mradi kwa wakati.
Pamoja na hayo RC Makonda amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya NAMIS Corporate LTD inayojenga Soko la Tandale kukamilisha ujenzi huo haraka ili wafanyabiashara wauze bidhaa katika sehemu nzuri.
Post a Comment