Mpinzani wa Bondia Mwakinyo kutua nchini Novemba 18, 2019
Bondia Hassani Mwakinyo akimtandika Mwingereza Sam Eggington katika raundi ya pili.
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Mpinzani wa Bondia Hassani Mwakinyo, Mfilipino Arney Tinampay anatarajia kuja nchini Novemba 18 mwaka huu kwa ajili ya pambano la raundi 10 la Super Water kilo 69 linalotarajiwa kufanyika novemba 29 katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam.
Mfilipino Tinampay ni bondia namba moja katika uzito kilo 69 nchini Ufilipino na ameonekana kuwa mzuri katika ulimwengu wa masumbwi kutokana na takwimu zinaonyesha katika mapambano 51 aliyocheza hajawai kupoteza kwa KO.
Akizungumza na waanydishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Promota Jay Msangi, amesema kuwa bondia Tinampay anatarajia kuja nchini akiwa na timu ya zaidi ya watu watatu kwa ajili pambano dhidi ya bondia Mwakinyo.
"Bondia Tinampay atakuja nchini siku 10 kabla ya pambano, kujakwake mapema inaonyesha amejiandaa vya kutosha kuelekea katika mchezo huo, ambapo asilimia kubwa ya mashabiki wanasubiri" amesema Promota Msangi.
Promota Msangi amesema kuwa kutokana na ubora wa bondia Tinampay, tayari kituo runinga cha Taifa nchini Ufilipino wameonesha nia ya kurusha mubashara pambano hilo ambalo linaendelea kuteka mashibiki wa ngumi ulimwenguni.
Akizungumzia maandalizi ya Bondia Mtanzania Mwakinyo, Promota Msangi ameeleza kuwa kwa sasa anaendelea na mazoezi ili kuhakikisha anampiga mpinzani wake katika raundi za awali.
"Mwakinyo amekataa kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo, amesema yeye akiwa hapa nchini ameona ni mazingira rafiki kufanya mazoezi kuelekea mchezo huo" amesema Promota Msangi.
Promota Msangi amefafanua kuwa kuna bondia kutoka Afrika kusini anatarajia kuja nchini kwa ajili kumpa uzoefu Mwakinyo kuelekea katika pambano hilo la Kimataifa.
Amesema kuwa bondia kutoka Afrika kusini katika kupigana kwake anafanana na Mfilipino Tinampay, hivyo tumeona ni vyema kujifunza mbinu za kumpiga mpinzani wake.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST) Bw. Anthony Luta, amesema kuwa Mwakinyo ni bondia mwenye kipaji, hivyo anaamini siku ya novemba 29 atampiga mpinzani wake.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST) Bw. Anthony Luta akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa nachotakiwa kufanya bondia Mwakinyo kuwa na utilivu kuelekea pambano hilo kitu ambacho kitamsaidia kupata matokeo.
Hata hivyo wadau mbalimbi wa ngumi wameonyesha kuwa na matumaini na bondia mtanzania Mwakinyo kumpiga mfilipino Tinampay.
Msanii wa filamu Steve Nyerere, amesema kuwa katika pambano hilo bondia Tinampay atapigwa na Mwakinyo katika raundi ya tano hadi atatapika nyonga.
"Kama bondia Mwakinyo akipigwa mimi naacha kazi yangu ya usanii" amesema Steve Nyerere.
Katika mchezo huo kimataifa kati bondia Mtanzania Mwakinyo pamoja Mfilipino Tinampay utakaopigwa katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam siku ya novemba 29 mwaka huu, tayari Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepelekewa mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo la kistoria.
Tinampay ana rekodi ya kucheza mapambano 51 na kushinda 26 (12 kwa KO), amepigwa mara 24 zote kwa pointi na kutoka sare mara moja wakati Mwakinyo ambaye ni bondia wa 19 wa dunia kwenye uzani wa super welter amepigana mapambano 17 na kushinda 15 (11 kwa KO) amepigwa mara mbili (moja kwa KO) hajawahi kutoka sare.
Post a Comment