Ads

MAKONDA AKABIDHI ENEO LA UJENZI HOSPITAL YA WILAYA UBUNGO , AWAPA MIEZI 3 JKT KUKAMILISHA UJENZI.



Na John Luhende
Siku chache baada ya Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuridhia ombi la mkuu wa mkoa wa Dar es salaamPaul  Makonda  la kupatiwa  sh. Bilioni 1.5  kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ubungo amekabidhi eneo lenye hekari 5 kwa Jeshi la Kujenga taifa(JKT) kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukagua eneo hilo lililopo Kata ya Baruti  Kimara Dar es Salaam , Makonda  amemshukuru Rais Magufuli kwa  kuridhia ombi lake  na katika kuharakisha ujenzi huo amekabidhi kazi  ya ujenzi kwa Jeshi la kujenga Taifa  ambapo wamekubaliana kujenga kwa muda wa miezi mitatu .
“Rais Magufuli aliniambia anataka hospitali ijengwe ndani ya miezi mitatu ikamilike.Nikamwambia JKT ndiyo watakaoijenga hivyo leo(jana) nalikabidhi eneo chini ya uongozi wa Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Charles Mbuge,”alisema.
Alisema Rais anataka wananchi wa Ubungo wapate huduma za afya haraka iwezekanavyo kwani alipoingia madarakani miongoni mwa kipaumbele chake kilikuwa ni afya.
Makonda alisema Rais aliridhia ombi lake dhidi huduma za afya katika Wilaya hiyo ambayo ni mpya hivyo inahitaji viogozi shupavu wenye kuhitaji maendeleo.
Alisema serikali ilishatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ambacho tayari kinatumika kutoa huduma huku Wilaya ya Ubungo ikitumia hospitali ya palestina kama hospitali ya Wilaya.
“Katika upande wa Afya ilionekana haina vigezo vya kufuzu kuitwa hospitali ya Wilaya, hivyo Wilaya ya Ubungo ikabaki kuwa haina hospitali,”alisema.
Alisema wananchi wa Jimbo la Ubungo hawajapata viongozi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi bali imepata viongozi kwa ajili ya matumbo yao.
Aliongeza kuwa serikali ya Chama cha Mapinduzi ipo kwa ajili ya maendeleo na kubainisha kuwa Rais Magufuli hawezi kujua kila kitu na ndiyo maana anahitaji wasaidizi waliochaguliwa na wananchi husika kuwasemea .
“Bahati mbaya Ubungo hamna watu hao, mlipoteza.Nawapa pole kwasababu najua hata changamoto ya maji aliyeipigania ni Rais Magufuli ndiyo maana leo Ubungo mnamaji,”alisema.
Makonda aliwataka wananchi hao kutowaonea haya walafi na wanaojineemesha  kupitia fedha zao huku wakishindwa kupaza sauti kwasababu ya kupata huduma bora zaidi.
Alisema anafahamu kuwepo kwa sehemu zenye changamoto za barabara lakini viongozi waliowachagua hawawasemei bali kuhamia mtandaoni bila kujali wananchi waliowachagua.
“Mimi ndiyo msimamizi wa miradi  Dar es Salaam, hakuna kitabu cha bajeti Ubungo mwaka wowote ule kikisema kimetenga sh bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga hospitali ya Wilaya na mimi ndiyo naibeba bajeti kuwapelekea wabunge Dododoma,”alisema.
Makonda aliongeza “Wakati wa kudanganywa umepita ni wakati wa kuchapa kazi wala si maneno, endeleeni kumuunga mkono Rais wetu na kupitia fursa hii mchague viongozi wa mtaa wanaojitambua watakaounganisha nguvu ya Rais Magufuli wasemaji wa wananchi ili tupate maendeleo kwa pamoja,”alisema.
Kwaupande wake mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic  alisema eneo hilo limekuwa dogo kutokana na uhaba wa maeneo na kwamba watajitahidi kuchora michoro ya majengo kulingana na ukubwa wa eneo hilo, kulingana na mwongozo wa serikali  hospital ya Wilaya inatakiwa kujengwa katika eneo lenye ukubwa usio pungua ekeli 30.
Nao baadhi ya wananchi waliofika kuona eneo hilo  wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwakumbuka wananchi wa Ubungo  kwa kuwajengea hospital ya wilaya huku wakimpongeza RC Makonda kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za afya bila kujali kuwa Manispaa hiyo inaongozwa na Chama pinzani.


No comments