ACHA, TRW, SAHRINGON waungana kupinga ubaguzi Afrika Kusini
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Taasisi zisizo za kiserikali ya Action for change(ACHA), The Right way (TRW) pamoja na Mtandao wa Mashirika ya kutetea Haki za Binadamu kusini mwa Africa (SAHRINGON) zimetoa wito kwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. John Pombe Magufuli kuchukua hatua ya kukomesha ukatili unaofanywa Afrika kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa tamko la hilo Kiongozi Mkuu wa Mtandao wa Mashirika ya kutetea Haki za Binadamu kusini mwa Africa (SAHRINGON) Bi. Martina Kabisama, amesema kuwa nchini Afrika kusini kumekuwa wimbi la kuwashambulia wageni kitu ambacho sio rafiki kwa Afrika.
Amesema kuwa kutokana na kuongezeka Kwa matukio ya kibaguzi ni vizuri mwenyekiti wa SADC Dkt. Magufuli akachukua hatua ili kuhakikisha vitendo vya ubaguzi vinaondoka.
"Uzalendo ambao uliasisiwa na mataifa ya Afrika na mababa wa Afrika umevamiwa na kuufanya uzalendo usinyae" amesema Bi. Kabisama.
Ameeleza kuwa wakati umefika waafrika kwa pamoja waungane na kuainisha zaidi cha ubaguzi ambao watu na mataifa mengine wakiendelea kubaguliwa.
Amesema kuwa ACHA, TRW na SAHRINGON wanatambua kuwa Tanzania ndiye Mwenyekiti wa SADC ambapo matukio ya kibaguzi yanatendeka.
"Tunayo imani na Rais Dkt. Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa SADC kuitumia fursa hiyo kumaliza sintofahamu pamoja na vituko vinavyoendelea Afrika ya kusini" amesema Bi. Kabisama.
Amesema kuwa kinachotokea kwa kaka na dada zetu ni nchini afrika kusini wanaumia kwa kiwango kikubwa kwa kunyanyapaliwa utu wao, haki zao za kibinadamu pamoja na fursa za maendeleo yao.
Imeelezwa kuwa ni busara viongozi wa afrika na serikali zao wakanyamazisha kukomesha aina hii ya ubaguzi wa utaifa ambao ni ukatili, unyanyapaa, vitendo vya kupangwa na ukatili wa kuzaliwa na ulio moyoni.
Katika hatua nyengine ameeleza kuwa wakati umefika wa kuvunja mnyororo wa ubaguzi, kutengwa.
"Raia wa afrika tunapaswa kusimama kupigania amani endelevu na utulivu milele" amesema Bi Kabisama.
Post a Comment