MIRADI YA KIMKAKATI KUONGEZA MAPATO YA TAMISEMI.
Mwambawahabari
Na Ismail Ngayonga
SERIKALI kupitia
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inatekeleza
Mkakati maalum unaolenga kuziwezesha Halmashauri kujitegemea kimapato ili kutoa
huduma bora zaidi na zenye uhakika kwa wananchi.
Katika kutekeleza
Mkakati huu, Wizara ya Fedha na Mipango imetoa maelekezo kwa Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatumia kwa ukamilifu fursa za kimapato
zilizopo katika maeneo yao na hivyo kuongeza uwezo wa kujitegemea kimapato.
Takwimu zinaonesha
kuwa bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa hutegemea ruzuku kwa zaidi ya
asilimia 88 kutoka Serikali Kuu katika kuchangia utekelezaji wa bajeti pamoja
na kugharamia utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Kwa kuzingatia sababu
hizo, Wizara ya Fedha na Mipango imeanzisha utaratibu kwa Halmashauri
mbalimbali nchini kufanya mawasilisho ya miradi yao ya kimkakati katika eneo la
kujijenga kimapato kwa madhumuni ya kujitegemea na kuboresha utoaji wa huduma.
Msingi wa utaratibu
huu unatokana na ukweli kwamba upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye
uhakika katika Halmashauri ni nguzo imara katika kuboresha utoaji huduma nzuri
na zenye uhakika kwa wananchi.
Akiwasilisha
Makadirio ya Hatuba ya Bajeti kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo anasema
Ofisi ya Rais TAMISEMI ilianza utaratibu
wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika Mwaka wa Fedha 2017/18.
Anasema miradi hiyo inapaswa kuwa na sifa ya kuiwezesha Halmashauri
kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuziwezesha kujitegemea kimapato na
kupunguza utegemezi wa Ruzuku ya Serikali Kuu.
Anaongeza kuwa hadi Februari, 2019 jumla ya Halmashauri 29 zenye miradi 37 zimekidhi vigezo vya kupatiwa jumla ya Tsh Bilioni 268.84 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya
kimkakati ambapo katika awamu ya kwanza Halmashauri 18 zenye miradi 23 zilikidhi vigezo vya kupatiwa jumla ya
Tsh Bilioni 131.46.
“Kati ya Fedha hizo Tsh
Bilioni 31.36 zimepokelewa kwenye
Halmashauri hizo ambazo zimesaini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya
kimkakati zitakazotumika kutekeleza miradi ya ujenzi wa masoko, viwanda,
machinjio, vituo vya mabasi na maghala ya kuhifadhia mazao” alisema Jafo.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo anasema katika Awamu ya Pili, Halmashauri
nyingine 12 zenye miradi 15 zimekidhi vigezo vya kupatiwa jumla ya Tsh Bilioni
137.37 mwezi Januari, 2019 na
kusaini mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo itakayohusisha ujenzi wa masoko
ya kisasa, machinjio ya kisasa, vituo vya mabasi, uendelezaji wa ufukwe wa
Oysterbay.
Waziri Jafo anasema Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara
ya Fedha na Mipango inaendelea kujenga uwezo kwa Halmashauri kuziwezesha kuibua
miradi, kufanya upembuzi yakinifu ili miradi hiyo iweze kukidhi vigezo na
kupata fedha na kuitekeleza kwa ufanisi.
Upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye uhakika katika Halmashauri ni
nguzo imara katika kutatua changamoto za mapato katika ngazi ya halmashauri ni
pamoja na uwezo mdogo wa kubaini na kutumia fursa zilizopo pamoja na usimamizi
hafifu katika ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya mapato ambazo zina athari
katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Matumizi mazuri na yenye tija ya fursa hizi katika vyanzo vya mapato
yataziwezesha Halmashauri kuwa na vyanzo vya uhakika ili kujijengea uwezo wa
kujitegemea na hivyo kuiwezesha Serikali Kuu kuongeza nguvu na msukumo katika
Halmashauri zenye uhitaji zaidi.
Post a Comment