Wananchi Rukwa kushiriki kuchangia Damu kusaidia Majeruhi ajali ya Morogoro
Mwambawahabari
Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
..............................................
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi
wa mkoa huo kushiriki katika zoezi la kuchangia damu litakalofanyika kwa muda
wa siku tano kuanzia tarehe 14 hadi 18.8.2019 katika halmashauri nne za mkoa, ili
kusaidia majeruhi walioungua na moto uliosababishwa na kulipuka kwa lori la Mafuta
katika ajali iliyotokea eneo la Msavu mkoani Morogoro, na kusababisha vifo vya
watu 76 na majeruhi 54.
Mh. Wangabo amesema kuwa zoezi hilo litawajumuisha Waendesha
Bodaboda na Bajaji, Madereva wa Magari, Vijana, Watumishi wa Serikali, Wanafunzi,
Vyama za Siasa, Madhehebu ya Dini, Viongozi mbalimbali na wale wote wenye
mapenzi mema na moyo wa kujitolea kwaajili ya majeruhi hao.
“Nafahamu kuwa mtu yeyote aliyeungua sehemu yoyote ya
mwili, miongoni mwa madhara makubwa anayoyapata ni pamoja na kupoteza kiasi
kikubwa cha maji mwilini (Dehydration) na kupungukiwa damu mwilini (Anaemia). Kwa hiyo natoa wito na kuwaomba Wananchi wa
Mkoa wa Rukwa kuchangia Damu kwa ajili ya wenzetu majeruhi wanaoendelea na
matibabu. Damu hiyo pamoja na salamu
zetu za pole tutaiwasilisha kwa Dkt. Kebwe Steven Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro,” Alisema.
Aidha
Mh. Wangabo kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Rukwa anaungana na Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole kwa
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Viongozi wa Mkoa huo, Familia za Marehemu,
Ndugu, Jamaa na Marafiki kwa kuondokewa na Wapendwa wao. Na kumuomba Mwenyezi Mungu awape Moyo wa
Subira na Uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
“Mungu
awape pumziko la milele waliopoteza uhai na awaponye Majeruhi wote wanaoendelea
na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na hospitali ya Rufaa
Mkoa wa Morogoro. ‘Bwana Alitoa na Bwana
Alitwaa Jina lake lihimidiwe’.” Alimalizia.
Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo kabla ya kuanza kwa
kikao cha baraza la madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kilichohusu
utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa
hesabu za serikali nchini.

Post a Comment