TAFITI: ASILIMIA 99 YA WANAUME KUWATENGA WENZA WAO
TAFITI zinaonyesha idadi ya wanaume wanaohudhuria kliniki kuwasindikiza wenza wao wakiwa wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano imezidi kuongezeka tofauti na miaka ya nyuma.
Takwimu iliyotolewa hivi karibu wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Seleman Liwowa wakati akifungua mradi wa World Vision Tanzania (WVT), zilionyesha mahudhurio ya wilaya hiyo yameongezeka hadi kufikia asilimia 99 ambao huwasindikiza wenza wao pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Awali wanaume wengi walikuwa hawataki kuhudhuria kliniki wakiamini masuala hayo ni ya wanawake hivyo ongezeko hilo la uelewa litasaidia kutekeleza mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Hata hivyo Serikali inaamini ushiriki wa wanaume kliniki itasaidia kufahamu mapema afya ya mwenzi wake pamoja na mtoto anayemtarajia.
Wapo baadhi ya wanaume ambao walipenda kuwasindikiza wenzi wao kliniki lakini walikuwa wakikatishwa tamaa kwa sababu ya foleni na changamoto kadhaa zilizokuwa zikisababisha muda mwingine kukaa kliniki hata masaa zaidi ya tisa.
Hali hiyo ilisababisha wengi wao kuanza kusingizia kutingwa na shughuli mbalimbali za kijamii hivyo kuwaacha wenza wao wakihangaika pekee yao na pindi wanapomaliza ndipo huwasiliana ili waweze kuwafuata na wakati mwingine huondoka peke yao.
Anasema Serikali inaamini ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya afya ya uzazi yatasaidia pia kupunguza vifo vya wajawazito nchini.
Hali ya uzazi kwa Tanzania, Kenya na Uganda ikoje
Njia za kisasa za uzazi wa mpango baina ya wanawake waliopo kwenye ndoa wa umri wamiaka 15- 49 ni asilimia 32 (TDHS 2015/16), Hii ni ongezeko ukilinganisha na miaka kumi iliyopita toka asilimia 20 mwaka 2004/05 kufikia asilimia 27 mwaka 2010 .
Kwa wanawake waliopo kwenye ndoa wa umri wa miaka 15-49 ambao wanahitaji kuwa na nafasi kati mtoto na tototo lakini hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango ni asilimia 22 (TDHS 2015/16).
Pia kuna tofauti baina ya mikoa kuanzia ya chini sana ya asilimia 10 mkoa wa Lindi na ya juu kabisa ni Mkoa wa Kaskazini Pemba(Zanzibar).
Kwa vijana wa kike umri wa miaka 15-19 asilimia 42 hawajaweza kupata huduma ya afya uzazi (TDHS2015/16) na Tanzania ni moja ya nchi ambazo zina kiwango kikubwa cha mimba za utotoni duniani.
KENYA
Serikali ya Kenya pamoja na wadau wa
maendeleo wamefanya juhudi katika kuhakikisha afya ya uzazi inamfikia kila mwananchi, hali bado ipo chini ya kiwango kilichotarajiwa cha asilimia 53 katika mwaka 2005 na asilimia 62 mwaka 2010.
UGANDA
Wanawake walio katika umri wa kupata ujauzito, asilimia 51 wanatumia njia za uzazi wa mpango. Asilimia 47 wanatumia njia za uzazi wa mpango za kisasa, na asilimia 4 wanatumia njia za kuzuia uzazi za asili.
• Njia ya kuzuia uzazi ya sindano inatumiwa zaidi na wanawake waliopo kwenye umri wa kuzaa lakini hawajaolewa asilimia 21. na asilimia 14 wanatumia mpira wa kiume.
Utafiti uliofanywa katika vituo vya afya kadhaa na MTANZANIA ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mwananyamala , Amana na Mnazi Mmoja limeshuhudia idadi kubwa ya wanawake wakiwa pekee yao huku kukiwa na wanaume wachache ambao ndio wanawasindikiza wenzi wao.
Fikra potofu za awali kuhusu mahudhurio ya kliniki na nafasi ya mwanaume kuwa kazi yake ni kutungisha mimba, lakini kazi ya kuilea, kujifungua, afya na malezi ya mtoto ni jukumu la mke pekee yake inadaiwa pia huenda ni sababu ya wanaume kukwepa kwenda kliniki.
Said Jumanne Mkazi wa Wilaya ya Ilala anasema,yeye ni baba wa watoto watatu lakini awali alikuwa hajawahi kuongozana na mwenzake kliniki.
Anasema lakini wakati wanatarajia kupata mtoto wa tatu alilazimika kumsindikiza mkewe mara kwa mara kwa sababu alikuwa ana shida ya kiafya iliyokuwa ikimlazimu apate huduma nyingi kwa karibu.
"Kipindi hiki ndicho nilichobaini kuwa wanawake wengi wanateseka na wanahitaji Huduma za karibu za wenzao wao,"anasema Jumanne.
Pia anasema Ushiriki umesaidia kufahamu hali ya mama na mtoto mtarajiwa kiafya na yake binafsi.
Mkazi was Mbezi Irene Mushi anasema tangu aanze kupata ujauzito ambapo kwa Sasa ana watoto wanna hajawahi kuongozana na mumewe kliniki Jambo ambalo anasema ni hatari kwakuwa Ni rahisi hataumdanganya majibu ya vipimo mbalimbali hasa vya magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na zinaa.
AFP
Meneja utetezi kutoka shirika la kimataifa la Uzazi wa Mpango (AFP) , James Mlali anasema, kutokana na wanawake wengi kuelemewa na kulea wa familia kubwa wamekuwa wakishindwa kushiriki ipasavyo katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuongeza kundi la wategemezi.
Anasema hali hiyo imesababisha wanawake wengi kukosa fursa za kujiendeleza kiuchumi na kielimu.
Anasema kwa mwaka jana idadi ndogo ya wanawake waliweza kutumia njia za uzazi wa mpango ambapo asilimia 38 pekee ya wanawake nchini wakitumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.
"Asilimia 32 ya wanawake nchini wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango huku asilimia sita wakitumia za kienyeji," anasema Mlali.
Anaiomba serikali kuongeza nguvu katika suala hilo ili kuweza kupata asilimia 45 ifikapo mwakani.
Anazungumzia ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya uzazi wa mpango kwa nchini unaongezeka siku hadi siku kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali pamoja na Wadau katika kuinua ushiriki huo.
Anasema takwimu za kitaifa za 2015 zinaonyesha kwamba kwa wastani wa ushiriki huo umefikia asilimia 30.
Anasema Serikali imeweka malengo ya kuongeza ushiriki huo na mikakati maalum ya kufikia malengo hayo ikiwemo kutoa kipaumbele kwa wenza wanaoenda pamoja kwenye vituo vya huduma ambao hupewa nafasi ya kupata huduma bila kukaa kwenye foleni.
Anazungumzioa tembe za kuzuia uzazi kwa wanaume ambazo zimeanza kutumika nchini Marekani hapa nchini hazijaanza kutumika ambapo njia za Kisasa za Uzazi wa Mpango kwa Wanaume ambazo zinatumika na zimethibitishwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ni Mipira ya Kiume (Kondomu) na Kufunga Uzazi (Vasectomy).
Anasema njia zingine ambazo wanaume wanaweza kutumia ni zile za asili ambazo ni pamoja na kumwaga mbegu nje wakati wa kujamiiana (Withdrawal or Coitus Interruptus) na Kujizuia wakati wa siku za hatari (Abstinence).
" Hata hivyo, ufanisi wa njia hizi za asili ni mdogo sana na kuzifanya kuwa za kubahatisha,"anasema Mlali.
Anasema tafiti za kitaalam kuhusu njia za uzazi wa mpango zinaonyesha kuwa njia zote hazina uhusiano wowote na mtu kupungukiwa au kuishiwa nguvu.
Mlali anasema watu wanaopata matatizo kama hayo wanapaswa kuonana na wataalam wa afya ili wachunguzwe na kupata tiba husika.
Anasema wanaume wakishirikiana kwa pamoja na wenzi wao watasaidia kuongeza ufanisi katika matumizi ya njia hizo na kuinua hali ya maisha na furaha katika ndoa na familia.
Mlali anaelezea njia ya upasuaji kwa mwanaume kama njia ya kuzuia uzazi je akihitaji tena kupata mtoto anaweza.
Anasema njia ya kufunga uzazi kwa mwanaume (Vasectomy) inahusisha upasuaji mdogo usio na maumivu wala kusababisha majeraha makubwa.
Anasema njia hiyo, sambamba na ile ya kufunga uzazi kwa wanawake ni mahsusi kwa wale ambao wameridhika na idadi ya watoto na hawakusudii kuzaa tena.
Anasema njia zote za uzazi wa Mpango ni salama ila tofauti zilizopo ni katika ufanisi na muda wa matumizi.
Anasema njia za muda mfupi (Vidonge, Kondomu na Sindano) humtaka mtumiaji kuzirudia mara kwa mara. Kwa mfano: ni lazima kumeza Vidonge kila siku, kutumia Kondomu kila wakati wa kujamiiana, na kudungwa Sindano kila baada ya miezi mitatu ili kuepusha kutunga mimba.
Anafafanua kuwa njia za muda mrefu (Vipandikizi na Lupu) humkinga mtumiaji kwa miaka kati ya mitatu hadi mitano na ikishawekwa mwilini hufanya kazi wakati wote na kumhakikishia mtumiaji ulinzi anaohitaji hadi mwisho wa matumizi au akiamua kusitisha matumizi yake.
Anasema njia za kudumu (Vasectomy na Kufunga Uzazi kwa Mwanamke) zina uhakika wa moja kwa moja.
Anasema njia za Uzazi wa Mpango, kama zilivyo dawa zingine, zina maudhi madogo madogo (side effects) ambayo hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.
"Hivyo, ni vema mtu anapotaka kutumia njia hizi apate ushauri wa wataalam na vipimo ndipo achague njia itakayomfaa zaidi,"anasema Mlali.
Anasema ili wanaume waweze kushirikiana vyema na wake zao au wenza wao katika kipindi cha ujauzito hasa katika mahudhurio ya kliniki inabidi ,elimu kuhusu umuhimu na faida za ushiriki wao itolewe kwa kiasi cha kutosha.
Pia uhamasishaji wa kutosha ufanyike na mbinu mbalimbali kama vile motisha ya kuwapa kipaumbele cha kutosimama kwenye foleni zitumike,
Anasema ni vyema viongozi wa ngazi mbalimbali wahusike katika kuwahimiza wanaume kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na viongozi wa kiume nao wenyewe kuwa vielelezo.
Anaiomba Serikali katika ngazi ya taifa na halmashauri kutenga fedha za kutosha kugharamia utekelezaji wa mikakati hiyo.
Naye, Mkurugenzi wa utetezi AFP, Halima Sharrif anasema ufinyu wa bajeti kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango imekuwa ndicho kikwazo kikuu katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hapa nchini.
Anasema kuwa huduma za uzazi wa mpango zinahitaji sh. bilioni 20 kila mwaka katika kutekeleza.
‘Tafiti zinaonyesha kuwa Tanzania ni moja kati nchi zenye vifo vingi vitokanao na uzazi duniani, ambapo vifo 556 hutokea kwa kila vizazi hai 100,000; ikimaanisha kuwa zaidi ya wanawake 50 hufariki kila siku kutokana na matatizo ya uzazi’, anasema Halima.
MUHIMBILI
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya wanawake na uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk.Vicenti Tarimo anasema idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi imepungua kutoka vifo 125 mwaka 2017/18 hadi kufikia vifo 86 Julai nwaka 2018/ Juni Mwaka huu.
Anasema mwako wa wanaume kuhudhuria kliniki na wenzi wao bado ni mdogo.
Anasema kuhusu uzazi wa mpango kwa wanaume elimu bado inahitajika kwani wanawake wengi hawapo tayari kuona wanaume zao wanafanyiwa upasuaji mdogo kama njia ya kuzuia uzazi wakiamini kuwa hawatapata tena watoto.
"Wanawake wengi wapo tayari wao kuendelea kutumia uzazi wa mpango lakini si kwa wanaume zao wanaimani kwamba watakosa watoto moja kwa moja,"anasema Dk.Tarimo.
Anasema kwa hapa nchini bado tembe za kuzuia uzazi kwa wanaume hazijaanza kutumika ambapo njia zinazofahamika kwa sasa ni zile za awali zilizopitishwa na serikali.
Pia Mkuu wa Idara ya Ukunga na Uzazi wa Muhimbili, Mugara mahungururo, anasema wastani ya wanawake 15,000 hujifungua kwa mwaka kwa njia ya upasuaji na kawaida.
Anasema bado elimu sahihi ya uzazi wa mpango na ushiriki wa wanaume kliniki inahitajika ili wana ndoa waweza kupanga idadi ya watoto wanaowahitaji huku wakizingatia afya zao.
Post a Comment