Manispaa ya Ilala yatekeleza Miradi ya Maendeleo mwaka 2018/19 kwa asilimia 78
Mwamba wa habari
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala
imesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/19 imefanikiwa
kutekeleza Miradi ya Maendeleo kwa asilimia 78 huku ikibainisha kutenga Sh
bilioni 21.3 na kwamba kati ya hizo Sh bilioni 17.2 zimetumika katika
kutekeleza miradi hiyo.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam na Mchumi wa manispaa
hiyo, Ando Mwankuga katika Kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani wa Manispaa
hiyo kilichopitia na kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo katika kipindi cha
mwaka mzima.
Alisema katika kipindi cha fedha cha
mwaka huo manispaa ilitenga Sh bilioni 56.2 lakini ilivuka malengo kwa
kukusanya Sh bilioni 58 sawa na asilimia 102 hali iliyochangia
kufanikisha miradi hiyo kupata fedha ya kutosha.
Alibainisha kuwa katika
kipindi hicho cha bajeti manispaa ilitenga Sh bilioni 21.3 huku ikitumia Sh
bilioni 17.2 kukamilisha miradi ya ujenzi wa madarasa ya shule za msingi,
sekondari na vituo vya afya.
" Miradi ya elimu na afya
imetekelezwa ndani ya kipindi hicho ujenzi wa madarasa umesaidia wanafunzi wote
wa darasa la saba waliomaliza mwaka jana kujiunga kidato cha kwanza," alisema
Mwankuga.
Alisisitiza kuwa kiwango hicho cha
fedha kimefanikisha Ujenzi wa miradi ya madarasa ya shule za msingi na
sekondari pamoja na vituo vya afya kikiwemo Kituo cha Magonjwa ya Kuambukiza
kilichopo Kipawa.
Pia alisema mafanikio ya utekelezaji
miradi hiyo umechangiwa na utendaji kazi madhubuti wa Mkurugenzi wa manispaa
hiyo, Jumanne Shauri pamoja na ushirikiano kutoka kwa madiwani.
Katika hatua nyingine, Mwankuga alisema
manispaa hiyo imefanikiwa kutekeleza kwa asilimia 100 Ilani ya Serikali ya
Awamu ya Tano inayozitaka halmashauri zote kutenga asilimia 10 ya mapato kwa
ajili ya mikopo ya vikundi vya Vijana, wanawake na walemavu ambapo Sh bilioni
3.7 zimwetolewa.
Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ilala imeomba kutoa elimu ya rushwa kwa madiwani wa
baraza hilo ili kuwasaidia kutoa elimu kwa jamii wanayoiongoza.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudhibiti Ukimwi wa baraza hilo ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo,
Douglas Massaburi alisema katika kipindi cha mwaka 2018/19 watu 55,695
wamepatiwa huduma ya upimaji ya Virus vya Ukimwi huku akibainisha vifo 91
vimetokea.
Post a Comment