Ads

WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA ABAINISHA JITIHADA ZA SERRIKALI KWENYE MAPINDUZI YA KILIMO NCHINI


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa asasi zinazotoa huduma ndogo za fedha vijijini kwa Wajasiriamali Wadogo (TAMFI) katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 21 Februari 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa siku mbili wa wadau wa asasi zinazotoa huduma ndogo za fedha vijijini kwa wajasiriamali wadogo (TAMFI) wakifatilia hotuba ya waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akifungua mkutano huo katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 21 Februari 2019.
Rais wa VICOBA Endelevu Bi Devotha Likokola akiztoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi mara baada ya kufungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa asasi zinazotoa huduma ndogo za fedha vijijini kwa Wajasiriamali Wadogo (TAMFI) kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 21 Februari 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa asasi zinazotoa huduma ndogo za fedha vijijini kwa Wajasiriamali Wadogo (TAMFI) katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 21 Februari 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr. John Pombe Joseph Magufuli, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuweka mazingira bora ya kuleta mapinduzi katika kilimo.

Japokuwa Kilimo kinachangia karibu asilimia 30 ya Pato la Taifa, ukuaji wa Sekta ya Kilimo bado hauridhishi kutokana na changamoto zilizopo, japo kumekuwepo na mwelekeo chanya katika siku za karibuni. Kulingana na taarifa zilizopo za hivi karibuni ukuaji wa sekta ya kilimo umefikia asilimia 7.1

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 21 Februari 2019 wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa asasi zinazotoa huduma ndogo za fedha vijijini kwa Wajasiriamali Wadogo (TAMFI) katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania – Dar es salaam.

Alisema kuwa kwa kutambua hilo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo (ASLMs) kwa kushirikiana na wadau wa sekta inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme Phase Two-ASDPII).
Lengo kuu la ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (mazao, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.
Alisema kuwa Utekelezaji wa lengo hilo ni kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula; kuimarisha uchumi; kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda; na kuongeza ajira. Ili kufikia malengo haya; Utekelezaji wa ASDP II utazingatia mnyororo wa thamani wa mazao ya kipaumbele ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Alizitaja jitihada zingine katika kuleta mapinduzi ya kilimo ambazo ni Kuanzishwa kwa eneo maalum la kuboresha mnyororo wa thamani kwa mazao mbalimbali (yaani The Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT), Kuanzishwa kwa Program ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (yaani Marketing Infrastructure, Value Addition and Rural Finance Support Programme – MIVARF) ambao lengo lake kuu ni kusaidia nyanja mbalimbali muhimu katika kuendeleza kilimo cha kisasa nchini na Kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo (yaani TADB) ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wakulima na shughuli za kilimo nchini.
Alisema kuwa Jitihada za dhati zinahitajika kuwashawishi vijana kwa njia mbalimbali ili nao waingie katika biashara ya kilimo hasa katika uboreshaji wa mnyororo wa thamani kutokea shambani hadi kwa mlaji.

Kuwepo kwa huduma kama bima ya afya kwa wakulima na makazi bora kunaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kuwafanya watu wengi zaidi haswa vijana kujihusisha na kilimo kwa njia za kisasa zaidi na usalama wa afya zao na makazi yao pia.

Allisema kuwa hiyo itakuwa njia bora ya kutatua mahitaji yao na kuwasaidia wakulima vijana kufanya shughuli za kilimo pamoja na kilimo biashara kwa ufanisi. “Umefika wakati sasa tuhamasishe kuwa na Kilimo cha mashamba makubwa na ya kati yatakayopelekea kuzalisha kwa wingi na kwa tija” Alikaririwa Mhe Hasunga
Mkutano huo utafanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 21 Februari 2019 mpaka kesho tarehe 22 Februari 2019 ukiwa na lengo la kujadili namna bora ya kuwajengea wakulima uwezo wa kustahimili matukio mbalimbali kwa kutumia huduma za fedha vijijini, namna ya kuwanufaisha wakulima na huduma za hifadhi ya jamii, bima ya afya, matumizi ya teknologia rafiki ya kuwafikishia huduma za fedha vijijini, makazi bora kwa wakulima pamoja na elimu ya fedha vijijini.

Mkutano huo umewajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo maafisa kutoka serikalini, watoa huduma za kifedha vijijini, wataalam wa mambo ya kifedha, wakulima, na wawakilishi wa mashirika.


No comments