VALENTINE DAY IMEGEUKA KUWA SIKU YA UZINIFU...!
Na Mathias Canal
Ndugu zangu, Dunia nzima leo imetolea macho Siku ya
wapendanao (Valentine Day) ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 14 Februari
ya kila Mwaka.
Kwenye mitandao ya kijamii inaelekeza kuwa
Valentine Day imeanza karne ya 3 huko Roma ambapo alikuwapo padri aliyejulikana
kwa jina la St Valentinus aliyekuwa akiishi katika mji wa Roma wakati wa
utawala wa Claudis II.
Hata hivyo historia inaeleza kuwa Claudis alitaka
awe na jeshi kubwa huku akiamini kwa asilimia 100 kuwa vijana wangejitolea kwa
hali na mali na kujiunga na jeshi lake jambo ambalo lilikuwa gumu kidogo kwa
vijana hao ambao hawakupenda vita kwa kuogopa kama wangefia vitani maana yake
familia zao zingebaki na ukiwa mkubwa.
Pamoja na hayo Claudis alipiga marufuku kwa watu
kuoana kwa kuamini kwamba amekosa vijana wengi kwenye jeshi kwa sababu ya ndoa
zao imani ambayo pengine haikumsaidia kwani Askofu Valentine naye alikuwa
anawafungisha ndoa kwa siri vijana hao.
Claudis aliposikia kuhusu habari hizo za watu
kufungishwa ndoa kwa siri aliamuru Askofu Valentine akamatwe ambapo alihukumiwa
adhabu adimu kabisa kutokea ya Kifo cha kunyongwa.
Wakati akiwa jela Askofu Valentine alitembelewa
mara kwa mara na vijana mbalimbali ambao wao walikwenda kumsalimu huku
wakimpatia zawadi ya maua kuonyesha namna ambavyo walimthamini na kumjali na
kuonyesha wazi kuwa walikuwa pamoja nae.
Mmoja kati ya vijana hao waliomtembelea alikuwa ni
mtoto wa mkuu wa gereza ambaye yeye aliruhusiwa kuingia hadi Selo pasipo
kupingwa kama vijana wengine.
Wakati huo akiwa gerezani huku akisubiri kunyongwa
Valentine aliingia kwenye dimbwi la mapenzi dhidi ya binti huyo ambaye ni mtoto
wa mkuu wa gereza.
Hata hivyo muda mchache kabla ya kunyongwa
Valentine aliomba apatiwe kalamu na karatasi ili aandike ujumbe wake wa kuaga
ikiwa ni pamoja na kuweka sahihi yake. Ambapo aliandika "From Your
Valentine" (yaani Kutoka kwa Valentine wako)
Lakini siku ilikuwa imewadia pasina shaka Valentine
alinyongwa mpaka kufa tarehe 14 Februari Mwaka 269 BC ambapo baada ya kunyongwa
vijana wa Roma walianza kumuiga Valentine kwa kuwaandikia na kuwatumia wanawake
waliowapenda salamu za mapenzi.
Kuanzia siku hiyo Tarehe hiyo ikaanza kuhusishwa
zaidi urafiki, upendo na mahaba huku ikihusishwa zaidi na mapenzi. Lakini kadri
siku zinavyokwenda siku hiyo imezidi kuwa maarufu huku makampuni yakigeuza siku
hiyo kuwa ya biashara zaidi kwa kufanya kila kitu maalumu kwa siku ya
wapendanao kiwe na muonekana wa rangi yekundu kuanzia kadi za salamu, maua,
mpaka nguo wavaazo wapendanao inabidi ziwe nyekundu.
My Take
Nimeanza na historia ya Valentine kwa sababu kuu
mbili kwanza kuwafanya watu watambue kwanini wanasherehekea siku hii na ina
umuhimu gani kwao lakini pili kuwafanya watu watambue kuwa dhana ya Valentine
imepotoshwa kimaana.
Kwanza Valentine ni sherehe ya pili kwa umaarufu
Duniani ukilinganisha na sherehe ya Krisimasi ambayo ndiyo inatajwa kuwa nafasi
ya kwanza kwa umaarufu Duniani, hivyo umaarufu huu unachagizwa na watu ambao ni
wavivu katika kutafsiri mambo.
Lakini inawezekanaje kumchukia mtu ndani ya siku
365 halafu ukampenda kwa siku moja pekee...? Inawezekanaje kumpenda mtu
kuhusiane na rangi nyekundu ya nguo...?
Inawezekanaje kuamua kuadhimisha siku ya wapendanao
halafu ukajifungia chumbani na mpenzi wako kufanya uzinzi sasa itakuwa siku ya
wapendanao ama siku ya mapenzi.
Siku hii tunaitumia vibaya sana tofauti na maana
yaani leo hii mpenzi wako usipomwambia Happy Valentine Day anahisi humpendi kwa
kuwa ndivyo tulivyojiingiza kwenye maana isiyo yenyewe.
Leo ndio siku ambapo dunia inashangaza kwani ni
siku ambayo Nyumba za kulala wageni zitajaa wapenzi, leo ndio siku ambayo watu
wanaanzisha mahusiano mapya ya kingono, leo ndio siku ambayo Condom zitanunuliwa
kuliko siku zingine zozote zile, Zaidi leo ni siku ambayo kadi zitauzika kuliko
siku nyingine huku Club na Bar zikiuza zaidi.
Huu ni ulimbukeni wa kufikiri yaaani siku 365
unamchukia mtu halafu unakuja kujinasibu kwa mapenzi ya saa 24 hii ni dhambi
kubwa sana isiyo na kifani japo kwa mujibu wa dini ya kikristo dhambi zote ni
sawa.
Binafsi siku zote huwa ninawapenda ndugu, jamaa na
Rafiki zangu hakuna siku moja pekee ya kuwapenda.Lakini napenda zaidi watu
wapendane kwa moyo wa dhati sio kwa maigizo na ngono zembe.
Tusiangamie kwa kukosa Maarifa, kama tunaadhimisha
kumbukizi ya kufa kwa Padri Valentine basi kumbukizi yetu iwe na tafakuri
Chanya.
HAPPY VALENTINE'S DAY
Ni Neno La Wakati Mwema
Mathias Canal
0756413465
Ujiji-Kigoma
Post a Comment