Wanaowinda panya washauriwa kufuga kuku ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
Mwambawahabari
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewashauri
wananchi wote wanaoharibu misitu kwa kuchoma moto kwaajili ya kuwinda panya
waanze kufuga kuku ili kuweza kuokoa mazingira huku
akiwataka wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha
wanamuandalia mipango mikakati ya halmashauri zao katika upandaji wa miti ikiwa
ni kufuata agizo la serikali la kuitaka kila halmashauri kupanda miti milioni
1.5 kila mwaka.
Alisema kuwa moja ya matokeo ya shughuli hizi za
kibinadamu ni uharibifu mkubwa wa mistu na vyanzo vya maji unaoweza kusababisha madhara makubwa kama
kukosa mvua kwa wakati, uzalishaji mdogo wa chakula na hata maradhi mbalimbali
yanayotokana na uharibifu wa mazingira na kuongeza kuwa ufanisi wa zoezi hili la upandaji miti
unatia shaka kutokana na kutosimamiwa vizuri na Viongozi wa Halmashauri zetu
zote.
“Kwa hiyo naagiza
Wakurugenzi wote wa Halmashauri zetu kuwasilisha mpango mkakati wa upandaji
miti kwa kipindi cha Mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kubainisha idadi ya miti
waliyonayo na mahali ilipo pamoja na ya Wadau wao wa utunzaji wa Mazingira, na
maeneo ya kupanda. Mpango huu unifikie
ndani ya siku tano kuanzia leo,” Alisisitiza.
Vile vile alizitaka Taasisi za Serikali
kama shule, magereza na vyuo vya elimu kuanza kutumia nishati mbadala ikiwemo
ya “biogas” katika shughuli zao za mapishi ya chakula na kupunguza kasi ya
matumizi ya kuni kwani mkoa una mitambo 2 ya “biogas” katika Manispaa ya
Sumbawanga katika Vijiji vya Mtimbwa na Ntendo ambayo inatumika kama darasa la
kujifunzia ujuzi wa kutengeneza biogas
kutokana na mabaki ya mifugo yetu.
Wakati akisoma taarifa ya halmashauri
juu ya zoezi la upandaji miti, Afisa Ardhi na malisili wa halmashauri ya Wilaya
ya Sumbawanga Juma Chande alieleza kuwa katika msimu wa mwaka 2018/2019 katika
kata 8 kati ya kata 27, halmashauri imeshapanda miti 292,899 ambayo ni asilimia
17.4 ya lengo na ufafanua kuwa halmashauri inaendelea kutoa elimu ya kutunza
mazingira, kupanda miti na kilimo mseto huku akitaja changamoto zinazorudisha
nyuma juhudi hizo.
“Miongoni mwa changamoto ni muitikio mdogo
wa wananchi katika utunzaji wa mazingira pamoja na hamasa nyingi kutolewa kwao,
mila na tamaduni za wananchi za uwindaji wa panya mathalani kusababisha
uchomaji wa miti wakati wa kiangazi mfano maeneo ya vijiji vya Msandamuungano,
Sandulula na Mpwapwa hivyo kuathiri misitu iliyopandwa.” Alimalizia.
Post a Comment