Wamiliki wa Maabara Binafsi Wasiofuata Taratibu ,kubanwa.

Wamiliki wa maabara na vituo vya afya nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao mara moja bila shurti kabla ya Januari 15 2019 kwa kuhakikisha wanakamilisha vigezo vyote vya umiliki maabara hizo kwa kuwa muda wa kutoa elimu umepita na sasa ni muda wa kazi tu.
Akizungumza
na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya
afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto na Mkurugenzi wa bodi
ya usajili wa maabara Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa hadi kufikia
Septemba 2018 bodi ya usimamizi wa maabara binafsi ilitambua jumla ya
maabara 641 zinazojitegemea na maabara 719 zilizoshikizwa kwenye vituo
vya tiba vya watu binafsi vya ngazi mbalimbali.
Amesema
kuwa kutokana na baadhi ya wamiliki wa maabara binafsi hasa
zilizoshikizwa kutofuata maadili ya uwajibikaji kisheria kufikia
Septemba 20, bodi kupitia ziara yake imebaini kuwa kati ya vituo vya
tiba 1731vya watu binafsi vyenye maabara ndani ni maabara 1012 sawa na
asilimia 58 pekee ndizo zilizotimiza wajibu wake wa kujiandikisha kwenye
bodi ya usimamizi wa maabara binafsi na kutekeleza matakwa ya kisheria.
Amesema
kuwa wamiliki ambao hawatatekeleza wajibu wao wa kumiliki maabara hizo
watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kifungo pamoja na faini au
vyote kwa pamoja.
Amewataka
wamiliki hao kuhakikisha kuwa kila mmoja awe amekidhi vigezo vyote vya
umiliki wa maabara ikiwa ni pamoja na kulipa ada zote stahiki zikiwemo
malimbukizo ya nyuma na faini stahiki pamoja na kuwa na risiti halali za
malipo hayo. Pia amewataka wamiliki wa maabara hizo kulipa tozo stahiki
kila mwaka ili kuwezesha bodi kufanya uhakiki wa kudumu wa huduma
zitolewazo katika maabara hizo.
Vilevile
amesema kuwa katika kutekeleza hilo watatoa orodha za zahanati katika
gazeti la Serikali na zahanati isiyokuwapo kwenye orodha hiyo
haitatakiwa kutoa huduma yoyote na watakaokiuka watakutana na mkono wa
dola. Gwajima ametoa mwito kwa serikali katika ngazi zote kushirikiana
na kutoa taarifa dhidi ya wavunja sheria na kufanikisha kuipeleka
mbele sekta hiyo.
Akieleza
kuhusiana na faini zitakazotolewa Kaimu Afisa msajili wa bodi ya
usimamizi ya maabara binafsi Neema Halliye amesema kuwa kwa mujibu wa
sheria watakaokiuka sheria hiyo watapigwa faini ya kulipa kiasi cha
shilingi laki mbili au kufungwa miaka miwili au vyote kwa pamoja na bado
maboresho ya sheria hiyo yanafanyiwa kazi ili kuweza kutoa kibano
zaidi.
Post a Comment