"TUNATAKA TAIFA LA MABINTI WASOMI” DKT.NDUGULILE
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ameitaka jamii kuwawezesha watoto wa kike
kupata elimu ili kuwa na Jamii yenye mabinti wasomi na kuondokana na
ukandamizaji wa watoto wa kike na wanawake.
Dkt. Ndugulile ametoa rai hiyo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma
wakati akishirikiana na wananchi katika ujenzi wa Bweni la shule ya Sekondari
Mikalanga ambalo kwa kiasi kikubwa wananchi wametoa nguvu zao katika kufanikisha
ujenzi huo.
Dkt. Ndugulile amesisitiza kuwa suala la elimu kwa mtoto wa
kike na muhimu kutokana na changamoto za mtoto wa kike hasa suala la mimba za
utotoni ambazo zinapelekea kupotea kwa ndoto za wanafunzi wa kike wengi.
Naibu Waziri Ndugulile amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu
zilizopo Mtoto mmoja kati ya watoto watatu wa kike hupata mimba za utotoni na
kukatisha ndoto za Mtoto wa kike kupata elimu kati ya miaka 15 mpaka 19 ikiwa
sawa na asilima 27.
"Tunataka taifa la mabinti waliosoma, madaktari, wahandishi na wataalam wengine tuunge mkono
juhudi hizi ili tuondokane na na changamoto zinazopelekea watoto wa kike kupata
mimba za utotoni" alisisitiza Dkt. Ndugulile.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Ruvuma Mhe.
Jacquiline Ngonyani amemshukuru Naibu Waziri kwa kuamsha ari na kutoa mchango
wake wa mifuko 50 ya Saruji ili kufanikisha watoto wa kike kupata elimu na
kuondokana na changamoto za kukosa mabweni inayosababisha watoto wengi kupata
mimba.
Akitoa taarifa ya Mradi kwa niaba ya wananchi mjumbe wa
Kamati ya ujenzi wa Bweni hilo Inviolatha Lupogo amesema kuwa hadi kukamilika
kwa mradi huo utagharimu kiasi cha Shillingi 139 ambapo mchango wa wananchi
unatarajiwa kuwa ni Shillingi Millioni 43 na hadi sasa wananchi wamechangia
shillingi Millioni 11
Ameongeza kuwa lengo la mradi huo ni kupunguza adha ya
kutembea umbari mrefu , kuwapangisha watoto wa kike kiholela ambapo kwa mwaka
2017/2018 jumla ya watoto wa kike 12 walikatishwa masomo yao sababu ya ujauzito.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya ujenzi wa Bw. Lilbrad
Kinunda amesema kuwa wamefurahishwa na ujio wa Naibu Waziri Ndugulile na
kushirikina na wananchi katika ujenzi wa bweni hilo na wao wanaunga mkono
juhudi hizo kwa kujitolea katika kujenga
bweni hilo kwa amasa zaidi.
Katika kuuunga mkono juhudi za wananchi wa Mikalanga Naibu
Waziri Dkt. Ndugulile alitoa jumla ya mifuko 50 ya saruji na Mbunge wa
Viti maalum mkoa wa Ruvuma Mhe. Jacquiline Ngonyani amechangia jumla ya mifuko
30 ya saruji.
Post a Comment