Askari Polisi na Watuhumiwa Waliokuwa Wakitorosha Dhahabu Mwanza ,wasomewa mashitaka haya.

Askari polisi wanane wanaotuhumiwa kushiriki mpango wa kutorosha dhahabu kilo 319.59 zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 27 pamoja na wamiliki wa madini hayo, wamefikishwa mahakamani.
Washtakiwa hao waliokamatwa Januari 4, mwaka huu, walifikishwa mahakamani kwa makosa 12 likiwemo la uhujumu uchumi.
Walisomewa
mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa
Mwanza, Gwae Sumaye, na mawakili wa serikali Castuse Ndamgoba, Robert
Kidando na Jackline Nyantori.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa Januari 4, watuhumiwa wanne ambao ni Sajid
Abdallah, Kisabo Nkinda, Emmanuel Kija na Hassan Sadick walitenda kosa
la kuwapatia rushwa ya Sh. milioni 700 watuhumiwa wanne ambao ni askari
polisi ili kuwasaidia kutorosha madini hayo.
Askari
ambao majina yao yalitajwa na mawakili wa serikali ni Koplo Dani
Kasara, Koplo Matete Misana na makonstebo Japhet Kuliko, Maingu Sorry,
Alex Mkali, Timoth Paul na David Ngelela na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi
(SSP) Moris Okinda ambaye alikuwa kiongozi wa askari hao.
Miongoni
mwa mashtaka 12 yanayowakabili askari hao ni pamoja na uhujumu uchumi,
kuomba na kupokea rushwa ya Sh. milioni 700, kuisababishia hasara
serikali na kutakatisha fedha kinyume cha sheria za nchi.
Hakimu
Gwae alisema watuhumiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa sababu
mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliahirisha
kesi hiyo hadi Januari 28, mwaka huu, itakapotajwa.
Askari
hao wanane, kabla ya kufikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi Tanzania
liliwasimamisha kazi Januari jana kutokana na tuhuma za kutenda kosa
kinyume cha mwenendo mwema wa jeshi hilo.
Post a Comment