WANANCHI WASHAURIWA KUPIMA AFYA ZAO KABLA YA KUJIHUSISHA NA MICHEZO
Wananchi wameshauriwa kuchunguza afya zao kabla ya
kujihusisha na michezo au mazoezi mbalimbali ya viungo vya mwili ili
kuepukana na mstuko wa moyo unaoweza kusababisha vifo vya ghafla.
Rai
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati
akiongea na waandishi wa habari kuhusu vifo vya ghafla vinavyowatokea
wanamichezo wawapo uwanjani na wananchi wakati wa kufanya mazoezi ya
viungo vya mwili.
Prof.
Janabi ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema mshtuko wa
moyo huufanya moyo kuacha kufanya kazi inavyotakiwa na hii humtokea
mtu ambaye mfumo wake wa umeme wa moyo haufanyi kazi vizuri au mishipa
ya damu ya moyo imeziba.
Mtu
mwingine ambaye hukutwa na tatizo hili ni yule ambaye ana tundu kwenye
moyo, mishipa ya damu ya moyo kuwa na matatizo na hivyo kuchanganya
damu safi na chafu.
“Jamii
yetu imekuwa na tabia ya kufanya mazoezi mbalimbali bila kupima afya ya
moyo. Mazoezi yoyote yale ya viungo vya mwili husababisha misuli
kujijenga na kuwa mikubwa kama mtu ana ugonjwa wa moyo na misuli yake
imekuwa kutokana na mazoezi hupelekea kuziba kwa njia ya damu kutoka
kwenye moyo na kusababisha vifo vya ghafla”, alisema Prof. Janabi.
Aidha
Prof. Janabi ameviomba vyama vya michezo kushirikiana na hospitali
kubwa hapa nchini ili wakati wa michuano mbalimbali itakapotokea
mchezaji kupata tatizo la mshtuko wa moyo awapo uwanjani hospitali
hizo ziweze kumuhudumia kwa wakati na kuokoa maisha yake.
Kwa
upande wa vilabu vya michezo alivihimiza kufanya uchunguzi wa afya
ikiwemo afya ya moyo kwa wachezaji wao kabla ya kuwasajili ili kuepuka
kutumia fedha nyingi kusajili wachezaji ambao wana matatizo ya kiafya.
Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI )
Post a Comment