Ads

BAVICHA YALILIA WAFUASI WACHADEMA WALIOKAMATWA

Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limelalamikia  Jeshi la Polisi kuwazuia  wanachama wa chama hicho wanaofika mahakamani kufuatilia kesi zinazowahusu vigogo wa chama hicho.

Kufuatilia hali hiyo Bavicha wamemuomba Jaji Mkuu wa Tanzania na msajili wa mahakama kuingilia kati na kutoa tamko

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine saba wanakabiliwa na kesi mahakamani, mara nyingi inapotajwa, wanachama na wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania hujitokeza kwa wingi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 7, 2018 mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi amesema jambo hilo alilodai linafanyw ana polisi ni uvunjwaji wa haki za msingi za raia kufuatilia mashauri mbalimbali mahakamani.

Amesema tangu kesi inayowakabili vigogo hao ilipoanza kusikilizwa Machi, 2018 baadhi ya wafuasi wanaojitokeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu wamekuwa wakikamatwa na kuhojiwa.

"Bavicha tunachukizwa kwa kweli, jana polisi walitumia nguvu kubwa kuwazuia watu kusikiliza kesi za viongozi wetu na baadhi ya vijana wetu walikamatwa kwa saa kadhaa," amesema.

Sosopi amesema kufanya hivyo ni kuvunja sheria kwa kuwa wanaohudhuria kwenye kesi hizo si wafuasi wa Chadema pekee yao bali wapo wanaokwenda kwa ajili ya kufuatilia kesi za ndugu zao.

"Kwa mwenendo huu mahakama za kiraia zimegeuzwa kuwa Mahakama za kijeshi. Tunamtaka Msajili wa Mahakama na Jaji Mkuu kutoa tamko juu ya hali hii," amesema Sosopi.

No comments