TANI 240 ZA MAHINDI ZATAIFISHWA, ZAGAWIWA KWA YATIMA NA SHULE
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen.
Nicodemus Mwangela akimkabidhi mkuu wa shule ya sekondari ya Vwawa moja ya
magunia ya mahindi ikiwa ni sehemu ya tani 240 zilizogawiwa kwa shule 18 za
sekondari na vituo vya watoto yatima mara baada ya kutaifishwa na TRA kwa
kuingizwa nchini kinyume na taratibu.
Tani 240 za mahindi ya chakula
zilizokamatwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa kuingizwa nchini kutoka
nchi jirani kinyume na taratibu zimetaifishwa na serikali na kugawiwa kwa Vituo
vya watoto yatima na shule 18 za sekondari Mkoani Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen.
Nicodemus Mwangela amekabidhiwa mahindi hayo na kufikia uamuzi wa kuyagawa mara
baaada ya kujiridhisha kuwa yaliingia nchini kinyume na taratibu na sheria,
yametelekezwa kwa muda wa mwaka mmoja na wamiliki wake na bado yanafaa kwa
matumizi ya chakula.
“Mahindi haya kisheria
nimekabidhiwa baada ya wamiliki wake kushindwa kufuata sheria na taratibu za
nchi yetu, yalitoka nchi jirani na yalikuwa yanapelekwa nchi nyingine jirani,
TRA wameyataifisha na nimeona tuwagawie wanafunzi wetu na vituo vya watoto
yatima wapate chakula kwakuwa mahindi haya tumejiridhisha pia kuwa yanafaa kwa
chakula”, ameongeza.
Meneja wa Ushuru wa Forodha
wa Kituo cha mpakani cha Tunduma John
Masa amesema bidhaa zote zitakazobainika kusafirishwa kinyume cha
taratibu zitataifishwa kama walivyofanya kwenye mahindi hayo baada ya kubaini
kuwa yamesafirishwa kwa kukiuka sheria hivyo yamegawiwa kwa Mkoa ambao umetoa
kwa wanafunzi na watoto yatima.
Nao baadhi ya wakuu wa shule za
sekondari na wawakilishi wa vituo vya watoto yatima ambao wamepokea mahindi
hayo ya chakula wameipongeza serikali kwa msaada wa mahindi ambao utasaidia
upatikanaji wa chakula katika shule na vituo vyao.
Post a Comment