WANAHARAKATI WAPEWA ELIMU JUU MIKOPO YA BIASHARA NA MATUMIZI YAKE
Benki pamoja
na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na utoaji wa mikopo hapa nchini
zimetakiwa kuwa na kitengo maalum cha kumshauri mteja wake kabla ya kukopa, ili
kupunguza wimbi la wateja wanaofilisiwa baada ya kushindwa kurejesha pesa
wanazodaiwa na benki husika.
Wananchi kutoka kata mbalimbali za jiji la Dar es salaam wakifuatilia semina.
Hayo
yameelezwa na baadhi ya wananchi walioshiriki katika semina ya GDSS mapema
jijini Dar es salaam, ambapo wananchi wengi wamezitupia lawama benki nyingi kwa
kudai kuwa maafisa wake hawana utu wala huruma
katika kudai madeni yao.
Lakini pia
imeelezwa kuwa lugha inayotumiwa na benki zote sio rafiki kwa wateja wengi
kwani inasababisha wananchi kujiingiza katika majanga makubwa bila wenyewe
kujijua, na kuombwa ikiwezekana itumike lugha ya Kiswahili kwani sio wananchi
wote wanaelewa kingereza.
Mwananchi kutokea kata ya Kipunguni Selemani Bishagazi akichangia mada na kuonyesha msisitizo juu ya kile anachokiamini yeye.
Akiongea katika
semina hiyo Mwanaharakati kutoka Kipunguni Bw. Selemani Bishagazi alisema kuwa
kinachowaponza wananchi wengi ni kukopa kwa shida sio kukopa kwa malengo ya
kukuza au kuendeleza biashara ndio sababu inayowafanya kuyumba na hatimaye
kufilisiwa na benki au taasisi za mikopo.
Aliongezea
kuwa benki nyingi zinafurahia kuona mteja anashindwa kulipa deni ili wachukue
mali yake aliyoweka rehani, kwani kwa sasa taasisi nyingi za mikopo zinaangalia
kupata faida kubwa kupitia kwa wananchi wanyonge na wasiojua nini kimeandikwa
katika mkataba wanaouingia kati yao na benki na sio kuwasaidia.
Mwanaharakati Janeth Mawinza akitoa maoni yake kuhusiana hali halisi ya mikopo ya biashara mingi hapa nchini.
Kwa upande
wake Dada Janeth Mawinza kutoka Mwananyamara alisema kuwa kinachowaumiza
wanawake wengi ni kukosa elimu ya biashara kwani unakuta mwanamke anakopa pesa
baada ya kufanyia biashara anakwenda kulipia sherehe au ada ya mtoto shule bila
kuwa na mipango ya kuangalia atarejeshaje pesa hiyo na wakati haizunguki.
Lakini pia
kingine ni kwamba biashara moja ina mkopo zaidi ya mmoja mkopo wa kwanza
unachukuliwa ukishindwa kuendesha biashara anaenda kwenye benki nyingine
anachukua pesa kwenda kulipa deni na huo ukishindwa tena anakopa tena kuja
kulipa madeni ya nyuma hali inayofanya mkopaji kushindwa kwenda mbele na
matokeo yake kufilisiwa mali zake.
Na mwisho maafikiano
ni kuwa elimu itolewe kwa Maafisa Mikopo juu ya kuwaelimisha wateja wao na
namna ya kudai wateja wao, na elimu hii itolewe na Benki kuu ya Tanzania (BOT) ambao
ndio wasimamizi wakubwa wa taasisi za kifedha.
Post a Comment