Ads

Smiles Dental Clinic yafungua tawi jipya, yaishauri jamii kuzingatia afya ya kinywa




Hussein Ndubikile, 
Mwambawahabari.
Kliniki ya Smiles  Dental imefungua tawi jipya la kutolea huduma ya meno na kuishauri jamii kujenga utamaduni  wa kwenda kwenye vituo vya afya na hospitali kupima afya za meno yao angalau mara mbili kwa mwaka ili kujikinga na madhara ikiwemo kuoza meno,fizi,meno kutoboka pamoja na kutingishika.

Ushauri huo umetolewa  jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki  na Daktari wa kliniki hiyo  anayehusika na uzibaji meno yaliyotoboka, Sarah Isdore wakati akizungumza na kuwaonyesha wanahabari vifaa tiba vya kisasa vitakavyotumika kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa watakaofika kliniki hayo.

Amesema matatizo ya meno yamekuwa yakiwakumba watu kutokana na kutokuwa na utaratibu mzuri wa kuangalia afya za meno yao na kusisitiza kuwa matatizo hayo yanaonekana hasa kuwakumba watoto sababu ya kutopigishwa mswaki vizuri pamoja na kula vyakula vya sukari hali inayopekelea meno kuwauma na kutoboka.

" Angalau basi mtu mara mbili kwa mwaka atenge muda wa kuyaangalia meno yao hospitali au kituo cha afya ukifanya hivyo utapunguza matatizo yatokanayo afya mbaya ya meno," amesema.

Amebainisha kuwa ili kupunguza matatizo ya meno hasahasa kwa watoto wazazi wanatakiwa kuwafundisha watoto wao jinsi ya kupiga  mswaki vizuri na kutowapa vyakula hatarishi kwa meno.

Amesisitiza kuwa watoto wenye umri kati ya 5 hadi 10 ndio hasa wanasumbuliwa na matatizo ya meno kutokana na kutopewa uangalizi mzuri na wazazi wao.

Kwa upande wake, Muuguzi wa kliniki hiyo, Sara Hilu Bura amesema wamejipanga kutoa huduma bora kwa wagonjwa wataofika kliniki hapo kwani wana vifaa na mashine za kisasa za kutoa tiba ya meno.

Amefafanua kuwa matatizo ya meno yamekuwa sugu kutokana jamii kutokuwa na elimu sahihi ya afya ya kinywa (meno) na kwamba ameshauri ni vyema elimu ikatolewa kupunguza tatizo hilo.

No comments