Waweka Hazina, Wahasibu Watakiwa Kuzingatiai Matumizi Sahihi ya Fedha.
Mkurugenzi Msaidizi TEHAMA, Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Bartazal Kibola akifungua
mafunzo ya mfumo wa malipo (epicor 10.2) kwa Waweka Hazina na Wahasibu
(hawapo pichani) kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara,
leo Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bibi Beatrice Kimoleta
akitoa maelekezo ya mafunzo ya mfumo wa epicor 10.2 kwa Waweka Hazina
na Wahasibu (hawapo pichani) kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na
Manyara, leo Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea
jijini humo.
Meneja wa Mradi wa Mifumo ya Sekta za Umma
(PS3) Mkoani Dodoma, Bw. Gideon Muganda akitoa maelekezo kuhusu
ushiriki wa PS3 katika mfumo wa malipo (epicor 10.2) wakati wa ufunguzi
wa mafunzo ya mfumo huo kwa Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri
za Mikoa ya Arusha na Manyara, leo Jijini Dodoma.
Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa
ya Arusha na Manyara wakimsikiliza mgeni rasmi Mkurugenzi Msaidizi TEHAMA,
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Bartazal
Kibola (aliyesimama) ambaye alifungua mafunzo ya mfumo wa malipo (epicor
10.2) kwa niaba ya Mkurugenzi wa TEHAMA, Ofisi Rais TAMISEMI, leo Jijini.
Waweka Hazina na Wahasibu kutokana Mamlaka za zote za Serikali za Mitaa
wanajengewa uwezo wa kutumia mfumo huo utakaohusisha masuala yote ya
fedha ikiwemo mapato, matumizi pamoja na bajeti za Halmashauri husika.
Mfumo huo utaanza kutumika rasmi Julai 1, mwaka huu.
Na: Lilian Lundo – MAELEZO,
Dodoma.
Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Mamlaka za Serikali
za Mitaa nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zinazotumwa
katika Halmashauri zao.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi
TEHAMA, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Bw. Bartazal Kibola alipokuwa akifungua mafunzo ya mfumo wa malipo (epicor
10.2) kwa Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha
na Manyara. Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Wahasibu hao namna
ya kutumia mfumo huo ambao umeboreshwa zaidi.
“Mfumo huu mpya utakapoanza kutumika lazima sheria
na taratibu zifuatwe, matumizi ya fedha yaendane na bajeti ya Halmashauri
husika, vilevile ni muhimu kuhakikisha kuwa vifungu vyenu vya fedha
vinakaa vizuri,” alisema Kibola.
Aliendelea kusema, mfumo huo umerahisha kazi na kupunguza
gharama ambapo mabadiliko yote ya bajeti yatakuwa yakifanyika kupitia
mfumo huo tofauti na ilivyokuwa awali ambapo Halmashauri zililazimika
kutuma barua za mabadiliko ya bajeti ofisi za TAMISEMI.
Aidha, amesema mfumo huo utatatua baadhi ya changamoto
zilizokuwepo katika mfumo uliopita epicor toleo Na. 9.05 ikiwa ni pamoja
na changamoto ya kutoa taarifa za utekelezaji mara baada ya kufanya
matumizi kwa kuzingatia mipango iliyojiwekea Halmashauri husika.
Hivyo basi epicor toleo namba 10.2 itaondoa kabisa
tatizo la taarifa hizo kwani mfumo huo baada ya malipo kufanyika utakuwa
na uwezo wa kupeleka taarifa hizo kwenye mfumo wa mipango na bajeti
ambapo pia mfumo wa FFARS utakuwa umepokea taarifa hizo za matumizi
ya vituo na hivyo taarifa zote za utekelezaji kupatikana moja
kwa moja kutoka mfumo wa Plan Rep ambao pia umeunganishwa na mfumo wa
epicor 10.2.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za
Mikoa Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bibi Beatrice Kimoleta amewataka Wahasibu
hao kuingiza takwimu sahihi katika mfumo huo ili mfumo uweze kuongea
taarifa ambazo ni sahihi.
Vile vile, ameshukuru Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo
ya Sekta za Umma (Ps3) kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la
Marekani (USAID) kwa kuwezesha uboreshaji wa mfumo huo ambao utaleta
uwazi katika mapato na matumizi ya fedha za Umma katika Halmashauri
zote hapa nchini.
Mfumo wa malipo (epicor 10.2) unatarajiwa kuanza
kutumika katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini kuanzia Julai
1 mwaka huu. Mfumo huo utahusisha masuala yote ya fedha za Mamlaka hizo
ikiwa ni pamoja na mapato, matumizi pamoja na bajeti nzima ya Mamlaka
husika.
Post a Comment