WAGONJWA 20 WAFANYIWA UPASUAJI WA MOYO WA KUFUNGUA KIFUA KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU YA MOYO.
Jumla ya wagonjwa 20 ambao ni watu
wazima wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum ya
matibabu ya moyo ya siku sita
iliyofanywa na madaktari bingwa
wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya
Saifee ya mjini Mumbai nchini India .
Wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji wa
kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass
Grafting) tumefanya kwa wagonjwa nane (8), kubadili valvu mbili za moyo (Valve
Replacement) kwa wagonjwa 10, upasuaji wa kurekebisha mshipa mkubwa unaotoa
damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili (Aortic Aneurysm Repair/Bental
Procedure) na mgonjwa mmoja alitolewa damu iliyokuwa imeganda kwenye mshipa wa moyo (Blood Clot).
Wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji
hali zao zinaendelea vizuri na wote wameruhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na
kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu pamoja na kufanya mazoezi.
Ndani ya siku chache zijazo tutaanza kuwaruhusu baadhi ya wagonjwa ambao hali zao zimeimarika kurudi nyumbani.
Aidha katika kambi
hiyo iliyoanza tarehe 18 hadi tarehe 23 mwezi huu wa Juni kwa mara ya kwanza tumefanya upasuaji wa
kuvuna mshipa wa damu ndani ya kifua upande wa kulia na kushoto na kuunganisha
kwenye misuli ya moyo ili kuuongezea moyo damu.
Kambi hiyo pia ilienda sambamba na
utoaji wa elimu pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wageni na madaktari
wetu pamoja na wauguzi.
Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo
ni wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri hivyo basi
tunawaomba wananchi kujenga tabia ya
kupima afya zao mara kwa mara hii itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo
au la na kama wanamatatizo wataweza
kupata tiba kwa wakati.
Kutokana na matibabu ya moyo kuwa ya
gharama kubwa tunaendelea kuwasisitiza wananchi wajiunge na mifuko ya bima ya
afya ambayo itawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapohitaji
kutibiwa. Pia itasaidia Hospitali yetu kuendelea kujiendesha yenyewe kwa
kushirikiana na Serikali na wadau wengine.
Tunawaomba wananchi
waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa damu kati ya chupa sita
(6) hadi saba (7) wakati wanapatiwa
matibabu. Taasisi inamkaribisha
mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu ambao wanapenda kuchangia damu
waweze kufanya hivyo ili tuokoe maisha ya ndugu zetu wanaohitaji kufanyiwa upasuaji
wa moyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
27/06/2018
Post a Comment