Ads

Tanzania mwenyeji Mkutano Mkuu wa Majaji na Mahakimu Arusha


Hussein Ndubikile
Mwambawahabari
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Majaji na Mahakimu unaotarajiwa kufanyika mkoani Arusha kuanzia Juni 11 hadi 13 mwaka huu katika  Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Elieza Fereshi amesema mkutano huo utajadili mada na mijadala mbalimbali ikiwemo ya usawa wa kijinsia katika katika utoaji na upataji haki pamoja na washiriki kubadilishana uzoefu katika masuala ya utendaji.
“ Wageni wameshaanza kuwasili tunategemea majaji wakuu wengi kushiriki mkutano utafungua fursa kwa washiriki kujadili na kuweka mikakati itakakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa mahakama,” amesema.
Amebainisha kuwa katika mkutano mijadala na changamoto zitajadiliwa ili kupata maazimio yatakayoingiwa kwa pamoja na washiriki lengo likiwa kuwasaidia katika utendaji wao.
Amesisitiza kuwa suala la jinsia litajadiliwa kwa kuangalia jinsi gani haki za kisheria zinalindwa katika utoaji na upataji haki kwa kuwashirikisha wadau wa madawati ya jinsia na washiriki wa mkautano huo.
Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Catarina Revocati amesema mkutano huo utashirikisha nchi 51 za Afrika huku akibainisha kuwa siku ya kwanza kutakuwa na wajumbe 200 na kwamba siku zitakazofuata watafikia wajumbe 350 hadi 400.
Ameongeza kuwa katika mkutano huo mpango mkakati ni kuangalia suala la ufikiwaji wa haki kwa wote bila kujali jinsia.

No comments