WAZIRI MKUU MAJALIWA AKEMEA UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea uharibifu
wa makusudi
wa miundombinu ya barabara
na majengo unaofanywa na baadhi ya wananchi na kuwataka waache tabia hiyo mara
moja.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini
Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati
akijibu swali la Mbunge wa Magu, Bw. Kiswaga Destery aliyetaka kujua Serikali inachukua
hatua gani dhidi ya wananchi wanaoharibu miundombinu ili wakauze kama vyuma
chakavu kwa vile Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu hiyo.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatumia fedha nyingi sana kuboresha
miundombinu mbalimbali nchini na kwamba kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda
miundombinu hiyo.
“Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya
barabara na majengo ili kutolea huduma, Watanzania wote tunao wajibu wa
kuilinda na endapo itatokea mtu anaihujumu miundombinu hii, Serikali hatuwezi
kukaa kimya, lazima tutachukua hatua,” ameonya.
Amesema
jukumu la ulinzi ni la Watanzania wote, na kila Mtanzania anayo dhamana ya ulinzi
na usalama wa ndani ya nchi ikiwemo kuilinda miundombinu. “Juzi niliona kwenye televisheni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, Mheshimiwa Jaffo akishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani
Shinyanga, wamekamata Fuso lililojazwa vyuma vilivyong’olewa kwenye barabara,
ni vile ambavyo vinawekwa kwenye daraja na kingo za barabara,” amesema.
“Huu
ni uharibifu ambao hatuwezi kuvumilia, na katika hili Watanzania lazima
tuungane pamoja tukemee tabia hii. Tunatumia fedha nyingi kujenga kingo za
barabara, kuashiria maeneo yenye hatari lakini Watanzania wengine wanakuja
kung’oa kwa matumizi yao. Mimi naamini Mkoa wa Shinyanga utakuwa umechukua
hatua kali dhidi yao,” amesema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, MEI 17,
2018.
Post a Comment