SERIKALI YASAINI MKATABA WA KUWAKOPESHA WATUMISHI WA UMMA MITUNGI YA GESI NA VIFAA VYAKE.
Serikali imesaini mkataba na Kampuni ya Gesi ya Mihan Gas wa kukopesha mitungi ya gesi na vifaa vyake kwa watumishi wa umma.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni juhudi za Serikali za kutaka kupunguza matumizi ya mkaa pamoja na kuni kwa lengo la kutaka kuhifadhi misitu ambayo imekuwa ikitumika kama nishati.
Mkataba huo ulisainiwa jana Jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),Profesa Dos Santos Silayo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mihan Gas,Hamisi Ramadhan na huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Mej. Gen. Gaudence Milanzi akishuhudia tukio hilo.
Mbali na kusaini mkataba huo, TFS na Kampuni ya Mihan Gas zilizindua kampeni ya kukopesha mitungi ya gesi na vifaa vya vyake kwa Watumishi wa Umma.
Awali, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Milanzi aliwahimiza watumishi kuchangamkia fursa hiyo ya kukopa mitungi na vifaa hivyo kwani itasaidia katika kuokoa misitu.
“Hili ni tukio kubwa hasa kwa wale ambao ni watunzaji wa mazingira katika kuwezesha jamii kuanza kutumia nishati mbadala.’’ Alisema
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu zaTanzania (TFS),Profesa Dos Santos Silayo,alisema upatikanaji wa huduma hiyo ni jitihada za kuhakikisha matumizi ya mkaa yanapungua
Aliongeza kuwa nishati mbadala ndo njia pekee itakayosaidia jamii kuachana na matumizi ya mkaa na kuni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo,Hamisi Ramadhani aliishukuru Serikali kwa kuikubalia kampuni hiyo kusambaza gesi kwa watumishi.
Akizungumzia namna watumishi watakavyonufaika na mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji , Ramadhani alisema kampuni imetenga fungu ambalo litarahisisha ukopeshaji wa vifaa hivyo na kila Mtumishi atapewa nafasi ya kuweza kulipia mwezi mmoja mara baada ya kuanza kuitumia gesi.
Post a Comment