Ads

ZIARA YA KAMISHNA MKUU WA TRA KATAVI, YATATUA CHANGAMOTO ZA EFD


Na Rachel Mkundai, Katavi
Mwambawahabari 
Wafanyabiashara na mkoa wa Katavi wamefarijika na ujio wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Bw. Charles Kichere katika mkoa wao na kusema kuwa ziara hiyo imewasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kulipa kodi likiwemo suala la usumbufu toka kwa mawakala wa kuuza na kusambaza mashine za EFD kutokuwaletea mashine zao kwa wakati licha ya kuwa wamelipia takribani zaidi ya mwaka mmoja.
Wafanyabiashara hao wameyasema hayo mara baada ya kuzungumza na Kamishna Mkuu  wa TRA alipokutana nao katika ukumbi wa idara ya maji mjini Mpanda katika mwendelezo wa ziara yake ya kuhamasiha wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti EFD katika mikoa ya nyanda juu kusini pamoja na ile ya Magharibi mwa nchi.
Wafanyabiashara hao hawakusita kutoa shukrani zao kwa kusema kwamba ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA imekuja wakati muafaka kwa kuwa walikuwa na changamoto ambazo kwa muda mrefu ziliwafanya wasilipe kodi na kupitia mkutano huo wamepata fursa ya kumweleza na zimepatiwa ufumbuzi mara moja na zingine zilizobaki wana imani kuwa zitatatumliwa kwa wakati na sasa wapo tayari kulipa kodi stahiki.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, akizungumza mara baada ya kurudishiwa pesa na wakala wa EFD ambaye hakumpatia mashine yake kwa takribani miaka miwili, Bw. Kobra Kipara amesema awali alitapeliwa pesa na wakala wa mashine za EFD lakini Kamishna Mkuu amemtafuta wakala huyo na sasa amerudishiwa pesa zake.

Naye wakala wa uuzaji na usambazaji wa mashine za EFD wa kampuni ya Pegamon Bw.David Nyaga ameahidi kushirikiana na TRA kwa kuwasambazia wateja wake mashine za EFD kwa wakati na kuweka mikakati ya kuwafikia wateja wao katika mikoa yote kwa kufungua matawi ya ofisi zao na vile vile kutoa mafunzo ya namna ya kutumia mashine za EFD na kufanya matengenezo kwa wakati.

Hata hivyo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere ametoa wito kwa wafanyabiashara kote nchini kutembelea ofisi za TRA ili kupata tafsiri sahihi ya sheria za kodi na siyo kulipishwa kodi bila kuelewa.
Kamishna Kichere pia amewaagiza maofisa elimu kwa mlipakodi wa TRA katika mikoa yote kuwafuata walipakodi popote walipo na kuwapa elimu na tafsiri ya sheria za kodi ili kuongeza uelewa wa masuala ya kodi miongoni mwa wafanyabiashara na jamii kwa ujumla.
“Kama una shida, ni vema ukaenda kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato, pamoja na kwamba tunatoa elimu,lakini kama una shida, nenda ofisi ya TRA”, amesisitiza.
Bw. Kichere amesema kodi zinatozwa kwa mujibu wa sheria, sasa kunaweza kuwa na tafsiri ndogo ya kisheria au huelewi kitu, ametoa wito kwa wafanyabiashara kutembelea ofisi ya TRA ili kuapata uelewa mzuri wa kodi na siyo kulipa tu kodi ambazo hawazielewi.

No comments