WIKI YA ELIMU KWA MLIPAKODI KUFANYIKA TAREHE 5 HADI 9 MACHI, 2018
Na: Veronica Kazimoto
Mwambawahabari
Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi itafanyika tarehe 5 hadi 9 Machi, 2018 katika mikoa yote nchini ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea mrejesho na maoni mbalimbali kutoka kwa walipakodi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alisema wiki hii ya Elimu kwa Mlipakodi itakuwa inafanyika kila baada ya miezi mitatu ambapo pamoja na mambo mengine wananchi watapata fursa ya kuongeza uelewa juu ya masuala mbalimbali yanayohusu kodi.
"Katika wiki hiyo, mamlaka itafundisha mada mbalimbali kama vile ulipaji wa Kodi ya Majengo kwa njia ya kieletroniki ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha wamiliki wa majengo kulipa kodi hiyo kabla ya tarehe 30 Juni, 2018 ili kuepuka usumbufu," alisema Kayombo.
Kayombo alisema kuwa wafanyabiashara watafundishwa kwa undani juu ya Mkataba wa Huduma kwa Mlipakodi ambao umeainisha haki na wajibu wa mlipakodi na viwango vya huduma wanavyopaswa kupata kutoka TRA.
"Mada nyingine itakayofundishwa katika wiki hiyo ni pamoja na matumizi sahihi na umuhimu wa kutumia Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) ambapo wananchi watakumbushwa na kusisitizwa suala zima la kutoa na kudai risiti kila wanapouza au kununua bidhaa na huduma mbalimbali," alifafanua Kayombo.
Aidha, shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika wiki hiyo ni pamoja na usajili wa walipakodi wapya ikiwa ni moja ya dhamira ya TRA kuhakikisha kuwa, inasajili walipakodi wapya 1,000,000 nchi nzima katika mwaka huu wa fedha wa 2017/18.
Richard Kayombo ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika vituo ambavyo vimepangwa rasmi kwa ajili ya Wiki hiyo ya Elimu kwa Mlipakodi ili waweze kujifunza na kutoa maoni yao juu ya masuala mbalimbali yanayohusu ukusanyaji wa Mapato ya Serikali.
"Natoa wito kwa wananchi wote kutumia fursa hii ili waweze kujifunza kwa kina mambo mbalimbali yanayohusu kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ujumla," alisisitiza Kayombo.
Post a Comment