Ads

MFUMUKO WA BEI WAFUNGWA SPEED GAVANA

Mwambawahabari
Mfumuko wa bei wa taifa kwa Januari, 2018 umebaki kuwa asilimia 4 kama iliyokuwa Disemba,2017 kutokana na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kuwa sawa.

Ephraim Kwesigabo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam

Akizungumza Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Kijamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo amesema hali hiyo ni kutokana na kasi ya bei ya bidhaa za vyakula kuwa ile ile.


"Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Januari, 2018 imekuwa sawa na kasi iliyokuwa kwa mwaka ulioishia Disemba, 2017,"amesema.


Amesema mfumuko wa bei unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.


Kwesigabo amefafanua kuwa, bei ya bidhaa zilizochangia mfumuko wa bei kubaki kwa Januari, 2017 na Januari, 2018 ni mahindi kwa asilimia 8,maharage kwa asilimia 4.3,samaki kwa asilimia 9 na ndizi za kupika kwa asilimia 9.


Amesema baadhi ya bidhaa zisizo za chakula zilizochangia mfumuko wa bei Januari, 2018 ni pamoja na sare za shule kwa asilimia 2.3,huduma za afya hospitali binafsi kwa asilimia 10,mkaa kwa asilimia 9.4, vitabu vya shule kwa asilimia 2.7 na gharama za malazi kwa asilimia 3.2.


"Mfumuko wa bei usiohusisha vyakula vya nishati (Core Inflation) kwa Januari, 2018 umeongezeka kidogo hadi asilimia 1.4 kutoka asilimia 1.3 kama ilivyokuwa Disemba, 2017,"amesema.


Ameongeza kuwa, nchini Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Januari, 2018 umepungua kidogo hadi asilimia 3 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka unaoishia Disemba, 2017.


"Kwa upande wa Kenya, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Januari, 2018 umeongezeka hadi asilimia 4.83 kutoka asilimia 4.50 kwa mwaka uluoishia Disemba, 2017,"amesema.

No comments