Ads

Chadema wamkataa Msimamizi Uchaguzi Kinondoni


Mwambawahabari
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemkataa msimamizi wa uchaguzi wa ubunge jimbo la Kinondoni kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia taratibu za uchaguzi.

Pia, chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakikituhumu CCM  kuandaa mikakati ya kufanya vurugu siku ya uchaguzi huo, Februari 17.

Hayo yameelezwa leo Februari 6, 2018 na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Kigaila amesema mwenendo wa uchaguzi, hasa kamati ya maadili ya Kinondoni inayoongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli inasimamia mambo isiyoyahusu.

Amesema malalamiko yanayotolewa ni ya kijinai na hayawezi kufanyiwa kazi na kamati ya maadili, “Kimsingi kamati ya maadili haina uwezo nayo, yanapaswa kupelekwa polisi yenye jukumu ya kufanya uchunguzi.”

"Kamati ya maadili haishughulikii masuala ya jinai, watu wakipiga, wakipigwa wanashughulikiwa na polisi. Mkurugenzi ni msimamizi wa uchaguzi lakini amekuwa akiyashughulikia kinyume cha kanuni," amesema.

Amesema katika barua hiyo wameeleza mienendo ya mkurugenzi huyo wakidai kuwa si mizuri, “Hatumkubali, hatumtaki, aondolewe na tunapinga kwani hawezi kutenda haki.”

Amesema suala la jinai ambalo Kagurumjuli  analishughulikia ni la madai ya mwanachama wa CCM kupigwa na vijana wa Chadema, “Hatujajua hao vijana wanaotuhumiwa ni wa Chadema au la lakini hata kama ni kweli, mwanachama mmoja huwezi kuiwajibisha Chadema."

Katika mkutano huo, Kigaila amedai CCM wameanza  kuandaa vijana kufanya vurugu katika uchaguzi huo na  kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua.

"Tumeandika barua kwa IGP na NEC. Tumesema yeyote atakayejeruhiwa CCM iwajibike kwani imeanza kusambaza silaha, mashoka, nondo na mapanga," amedai Kigaila na kwamba barua hizo wanazipeleka leo katika taasisi hizo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Operesheni ya Kampeni Kinondoni, Frederick Sumaye amesema tuhuma hizo ana imani zitafanyiwa kazi.

Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema jitihada kubwa zinapaswa kufanyika nchini ili nchi kutoondolewa katika mfumo wa vyama vingi kwa madai kuwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi vinahakikisha wapinzani hawashindi.

"Tunaitaka NEC katika chaguzi hizi itende haki, Polisi wanaosimamia amani wote watende haki ili uchaguzi ufanyike kwa amani. Wasimamizi wa uchaguzi watende haki," amesema Sumaye.

No comments