WATOTO KUPIMWA SARATANI BURE
Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabari
Asasi ya Marafiki wa Watoto wenye Saratani Tanzania wameandaa huduma ya upimaji wa saratani ya watoto bila malipo itakayotolewa Februari 18 mwaka huu katika viwanja vya Donbosco vilivyopo Upanga, Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje – Marafiki wa Watoto wenye Saratani Tanzania, Janeth Manoni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utoaji wa elimu juu ya kansa ya watoto.
Bi. Janeth amesema kuwa saratani ya watoto ni janga kubwa ambalo wananchi wengi hawalifahamu kama linaathiri kwa kiasi kikubwa hivyo lengo la Asasi hiyo ni kutoa elimu juu ya ugonjwa huo.
”Utafiti uliofanywa mwaka 2015/2016 umeonyesha kuwa Tanzania tunategemea kuwa na watu 40,000 ambao watakutwa na saratani kwa kila mwaka ambapo kati yao watoto ni 2500 hivyo, janga hili ni kubwa kwa watoto na linahitaji kupewa kipaumbele ili kupunguza idadi yake”,alisema Bi. Janeth.
Ameongeza kuwa saratani za watoto zikigundulika mapema zina uwezo wa kupona kwa asilimia 80 lakini tatizo lilopo ni kucheleweshwa kufikishwa hospitali kwa sababu wazazi wengi hawafahamu dalili za awali za kansa hiyo.
Kwa upande wake Muasisi wa Asasi ya Saratani Tanzania Franklin Mtei, amesema kuwa wanaharakati wa sekta ya afya wamejitolea kutoa elimu juu ya dalili za saratani ya watoto kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kutoa elimu siku hiyo ya upimaji.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza siku hiyo na kujijengea utamaduni wa kupima afya mara kwa mara pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka kupata magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Post a Comment