DC KISARAWE ATAKA WANAWAKE WASHIRIKISHWE ARDHI YA FAMILIA INAPOUZWA
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe,
Happyness Seneda amewataka watendaji na viongozi wa vijiji vya wilaya
hiyo kuakikisha wanatoa vipaumbele kwa wanawake katika umiliki wa ardhi
na pia familia kuwashirikisha wanawake kutoa uamuzi pale wanapotaka
kuuza ardhi mali ya familia. Bi. Seneda alitoa kauli hiyo alipokuwa
akifunga semina kwa baadhi ya madiwani, watendaji na wenyeviti wa
Serikali za mitaa kutoka Wilaya ya Kisarawe iliyoandaliwa na Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP) kujadilia matokeo ya utafiti raghibishi uliobaini
uwepo wa migogoro mingi ya ardhi.
Kiongozi huyo amesema wanawake wengi wamekuwa wakiachwa nyuma
katika suala zima la umiliki ardhi na wakati mwingine hata familia
zimekuwa zikiuza ardhi kinyemela pasipo washirikisha wanawake jambo
ambalo si la kiungwana.
“…Wakati mwingine unakuta mume anaamua kuuza ardhi hata bila
kumshirikisha mkewe hili lazima viongozi mlisimamie, unapoletewa maamuzi
ya familia kutaka kuuza ardhi waulizeni wanaume je wamewashirikisha
wake zao katika uamuzi wa kuuza ardhi hiyo?,” alisema Bi. Seneda
akizungumza katika warsha hiyo.
Alitoa tahadhari kuwa endapo ataletea taarifa ya mwanamke
katika wilaya yake kudhuumiwa ardhi na kiongozi au mtendaji wa kijiji
kukaa kimya atahakikisha anaanza kumuwajibisha kiongozi kwa kufumbia
macho dhuluma hiyo. Hata hivyo alisisitiza kuwa wanawake wana haki ya
kumiliki ardhi kama ilivyo kwa wanaume hivyo viongozi wanapaswa
kulisimamia suala hilo vizuri ili kundi hilo lisinyanyasike katika
umiliki.
Aliwataka viongozi wa vijiji
kuhakikisha wanashirikiana na wananchi na viongozi ngazi za juu kutatua
migogoro ya ardhi ili kupunguza kero za wananchi na migogoro kati ya
wakulima na wafugaji katika maeneo hayo. Alisema uongozi wake kwa
kushirikiana na vyombo vingine wataendelea kufanya oparesheni za mara
kwa mara kuhakikisha wanawaondoa wafugaji ambao wamekuwa wakivamia
baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo na kulisha mifugo yao jambo ambalo
limekuwa likileta migogoro na uharibifu wa mazao ya wakulima.
Kwa upande wake, Bi. Bahati
Magendo mwakilishi wa wananchi Kijiji cha Vilabwa aliwatuhumu baadhi ya
viongozi na watendaji wa vijiji kuwapokea wafugaji kinyemela pasipo
husisha wananchi jambo ambalo limekuwa likiendeleza migogoro baina yao
na wafugaji. Alisema viongozi wamekuwa hawawashirikishi wananchi suala
la kupokea wafugaji vijijini jambo ambalo limekuwa chanzo kikubwa cha
migogoro. “..Viongozi wanatudharau wananchi hasa sie akinamama wamekuwa
hawatushirikishi katika maamuzi…utakuta mfugaji anakuja kijijini
anazungumza na kiongozi kimya kimya baadaye anahamia sisi hatuambiwi
chochote,” alisema Magendo.
Post a Comment