Waandaaji wa miswada ya filamu nchini watakiwa kuzingatia maadili ya kitanzania.
Mwambawahabari
Na Genofeva Matemu na Raymond Mushumbusi.
Waandaaji wa miswada ya filamu nchini wametakiwa kuhakikisha kwamba maudhui ya miswada inayoandaliwa inazingatia maadili na utamaduni wa Kitanzania ili kuifanya sera shirikishi inayoandaliwa kuwa na tija.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokua akifungua kikao cha Wadau wa Filamu kupitia uchambuzi wa hali ya Tasnia ya Filamu Tanzania kwa ajili ya ukamilishaji wa sera ya filamu na namna ya kuboresha filamu za ndani leo Jijini Dar es Salaam.
“Maudhui ya miswada ya filamu ikiandaliwa kwa kuzingatia maadili ya kitanzania itaboresha tamaduni zetu na kuzifanya kazi za sekta ya filamu kufanywa kwa kuzingatia weledi hivyo kuiona tasnia kama chombo kimojawapo kinachoisaidia Serikali sio tu kutoa burudani bali pia elimu kwa wananchi” amesema Mhe. Nnauye.
Aidha Mhe. Nnauye amesema kuwa mapinduzi ya sekta ya filamu hapa nchini yanawezekana iwapo kazi zake zitaonekana katika kiwango cha ubora kwa kuangalia maudhui yaliyomo na mapokeo yake kwa jamii.
“Napenda kuona wasanii wetu wanakuwa wabunifu badala ya kuwa na filamu zenye maudhui ya aina moja kwa kuzingatia weledi na kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kuweza kukidhi masoko ya filamu nje ya nchi” amesema Mhe. Nnauye.
Naye Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa kutokana na kukua kwa Tasnia ya Filamu kuna uhitaji wa Sera ya Filamu ili iweze kuwa dira ama mwelekeo na mwongozo katika kukuza tasnia hii na kuwezesha kuongezeka kwa fursa za uwekezaji, motisha na fursa za mitaji katika tasnia ya filamu nchini.
Bibi Fissoo amesema kuwa kukamilika kwa Sera ya Filamu kutabadidlisha kabisa taswira nzima ya Sekta ya Filamu hapa nchini kwani itaboresha uzalishaji wa bidhaa bora zenye kuzingatia weledi, filamu kuangaliwa kama chombo cha kukuza uchumi kwa manufaa ya Taifa na watanzania wote.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Bw. Methew Biko ameishukuru serikali kupitia Bodi ya Filamu na Idara ya Sera na Mipango kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wanatasnia wa filamu kuhitaji Sera ya Filamu na kuahidi ushirikiano wa dhati kutoka kwa wadau wa filamu ili kufanikisha uandaaji ya sera hiyo.
Kikao cha kupitia uchambuzi wa hali ya Tasnia ya Filamu Tanzania kimehusisha Wakurugenzi wa Idara, Wakuu wa Taasisi za Serikali na binafsi, wadau mbalimbali wa Tasnia ya Filamu wakiwemo wanazuoni, waigizaji, watayarishaji, waongozaji wa filamu, waandishi wa miswada, pamoja na wawekezaji.
Post a Comment