Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) umeondoa migogoro baina ya walimu na wazazi Mkoani Dodoma
Na: Lilian Lundo ,Dodoma
Mwambawahabari
Uanzishwaji wa Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) kwa shule za Msingi za Serikali Mkoani Dodoma umefanikiwa kutatua migogoro baina ya walimu na wazazi iliyodumu kwa muda mrefu mkoani humo.
Hayo yamesemwa leo, Mjini Dodoma na Mratibu Elimu Kata wa Kigwe Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma Elias Milaji katika Mkutano wa Waratibu wa Elimu Kata wa Mkoa huo kuhusu Mafanikio ya uanzishwaji wa UWW katika shule za Msingi za Serikali katika Mkoa huo.
"UWW umeweza kutatua migogoro mingi iliyoko katika kata ya Kigwe, moja ya migogoro hiyo ni wazazi kugoma kushiriki mikutano ya shule kutokana na walimu kukataa kuwafuta watoto wa kike shule ili wakaolewa," alifafanua Milaji.
Aliendelea kwa kusema kuwa, baada ya uanzishwaji wa UWW katika kata hiyo migogoro imepungua kwa kiasi kikubwa na wazazi wamekuwa wakishiriki katika kufuatilia maendeleo ya masomo pamoja na mahudhurio ya watoto wao.
Kwa upande wake Mratibu Elimu Kata wa Chamwino, Chitema Simango amesema kuwa UWW umewezesha kwa kiasi kubwa ushiriki wa wazazi katika maendeleo ya shule ambapo kabla ya uanzishwaji wa Umoja huo walimu walikuwa wakiachiwa ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi pamoja na shule lakini kwa sasa wazazi na walimu wanashirikiana kwa pamoja katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na shule.
Aidha UWW umeleta uwazi katika mapato na matumizi ya shule ambayo yanabandikwa katika mbao za matangazo za shule husika na wazazi wanapewa nafasi ya kuhoji juu ya mapato na matumizi hayo.
UWW ni mpango ulionzishwa na Serikali kwa kushirikiana na Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T) ukiwa na lengo la kuboresha mahusiano bora kati ya walimu na wazazi. Umoja huo mpaka sasa umeanzishwa katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mara na Lindi.
Post a Comment