Serikali ya Tanzania na China imesaini makubaliano ya ushirikiano wa masuala ya Uchumi.
Na Beatrice Lyimo
mwambawahabari
mwambawahabari
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano ya kikao cha tano cha kamati ya pamoja ya ushirikiano wa masuala ya uchumi, ufundi na biashara kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China.
Katika makubaliano hayo Serikali ya Tanzania imepokea kiasi cha shilingi Billioni 97 za kitanzania ambao utafadhiliwa na Serikali ya China kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu, Afya na Usalama kwenye viwanja vya ndege na Bandari nchini.
Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dar es salaam katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage pamoja na Naibu Waziri wa Biashara wa China Qian Keming.
Waziri Mwijage alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kusaidia Serikali ya Tanzania kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya Elimu, Afya, na Usalama wa Bandari na Viwanja vya Ndege ili kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na China uliodumu kwa muda mrefu.
Aidha, Waziri Mwijage alisema kuwa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya China imekubaliana kushirikiana katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo Serikali ya China imeahidi kutekeleza Mradi wa Mlandizi wa utengenezaji wa chuma unaotarajia kuanza wakati wowote.
Pia Serikali ya China imeahidi kujenga kiwanda cha Vigae katika eneo la Mkulanga ambacho kitakuwa na uwezo wa kutengeneza kilomita za mraba 80,000 kwa siku. Uzalishaji huo utaanza mara baada ya kukamilika kwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kinatarajiwa kuzinduliwa mwishoni mwa mwaka huu.
Vilevile amebainisha kuwa ifikapo mwaka 2019 Tanzania itaachana na uvaaji wa nguo za mitumba, hivyo Serikali ya China imeahidi ujenzi wa kiwanda cha nguo nchini chenye uwezo wa kuajiri wafanyakazi 14,000.
Naye Naibu Waziri wa Biashara wa China Qian Keming alisema kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwani imeshuhudia mabadiliko katika mbalimbali ikiwemo sekta ya miundombinu, viwanda na biashara hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika hatua nyingine Serikali ya Tanzania na China imesaini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi ambao utaiwezesha Serikali ya Tanzania kuimarika katika masuala ya Uchumi.
Mkataba huo umesainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dorothy Mwanyika na Naibu Waziri wa Biashara wa China Qian Keming unaolenga kuboresha mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo.
Mbali na hayo Serikali ya Tanzania na China imekuwa na majadiliano yaliyohusu uboreshaji wa Bandari ya Bagamoyo na maeneo yake kibiashara, nia ya kujenga Reli ya kati “Standard Gauge”, Bandari ya Zanzibar, Reli ya Tazara pamoja na Kiwanja cha ndege Zanzibar.
Post a Comment