SERENGETI NA BUNDA WANUFAIKA NA UWEKEZAJI WA SINGITA GRUMETI.
Mwambawahabari
Mfuko wa Singita Grumeti umeendelea kuwa mstari wa mbele katika
kuboresha hali ya elimu katika Wilaya za Serengeti na Bunda.
Hii imedhihirika kwenye halfa ya kukabidhi madawati 500 kwa Mkuu wa Mkoa
wa Mara Dk. Charles Mlingwa ili kupunguza uhaba wa madawati katika
Wilaya hizo. Aidha Grumeti wamekabidhi nyumba ya kuishi mwalimu
iliyojengwa katika Shule ya Msingi Makundusi.
“Tuko hapa kukabidhi madawati haya 500 yenye thamani ya Tshs Milioni 112
kwa Wilaya za Serengeti na Bunda pamoja na nyumba hii yenye thamani ya
Tshs Milioni 86” alisema Richard Ndaskoi ambae ni Mkuu wa Huduma za
Jamii toka Mfuko wa Singinta Grumeti.
Akipokea misaada hiyo, Dk. Mlingwa alisema “Nawashukuru Singita Grumeti
kwa Msaada huu wa madawati pamoja na nyumba hakika mchango wenu katika
Mkoa wa Mara unaoneka” Dk Mlingwa amewataka wawekezaji wengine katika
Mkoa wa Mara kuchangia madawati katika Wilaya za Serengeti na Bunda
kwani bado zina uhaba wa madawati.
Aidha Dk. Mlingwa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa
kuwa na mahusiano mazuri na wawekezaji waliopo katika Wilaya hiyo
“Tukiwawekea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao hata wananchi pia
watanufaika na uwepo wa wawekezaji hawa” alisema Dk. Mlingwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu pamoja na Mkuu wa Wilaya
ya Bunda, Lydia Bupilipili wote kwa nyakati tofauti wameushukuru Mfuko
wa Singita Grumeti kwa msaada huo wa madawati na kuuomba mfuko huo
kuendelea kuchangia katika shughuli za maendeleo katika Wilaya za
Serengeti na Bunda. “Wilaya hii ina wawekezaji wengi lakini wamekuwa
nyuma katika kuchangia shughuli za maendeleo, nawapongeza kwa kuwa
mstari wa mbele kusaidia jamii inayowazunguka pamoja na kuchangia katika
maendeleo ya Wilaya ya Serengeti” alisema Nurdin Babu.
Aidha Bi. Bupilipili ameuomba Mfuko huo kuanzisha kampeni maalumu ya
kuongeza kiwango cha ufaulu kwa watoto wa kike kwa shule za sekondari
Wilayani Bunda.
Singita Grumeti wamekuwa wawekezaji wenye tija kwa wananchi wa Wilaya za
Serengeti na Bunda licha ya kuwa mstari wa mbele kuchangia katika
shughuli za maendeleo, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa ajira kwa wakazi
toka wilaya hizo mbili pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi
toka wilaya hizo.
ENGLIBERT THOMAS KAYOMBO
AFISA HABARI NA MAHUSIANO
HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI
0763878804
Post a Comment