Kiwanda cha Chaki Wilayani Maswa kimehaidiwa mkopo wa shilingi milioni 30 kutoka mfuko wa vijana
Na: Genofeva Matemu WHUSM
Mwambawahabari
Vijana nchini wametakiwa kuiga mfano wa vijana wa Maswa Youth Family kuunganisha nguvu zao kuibua miradi yenye tija kwani heshima ya kijana ni kujitengemea na kulitegemeza taifa lake.
Hayo yamesema na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa Kiwanda cha Chaki Jana katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu.
Vijana wa Maswa Youth Family ni mfano bora wa kuigwa kwani ni vijana waliojitambua na kutambua yakua umoja ni nguvu hivyo kuchagua fungu lililo jema na kuwa mfano bora kwa wana Maswa na taifa kwa ujumla alisema Mhe. Jenista.
Aidha Mhe. Jenista amemuagiza Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana kuwakopesha tena vijana wa Maswa Youth Family shilingi milioni thelathini kutoka katika mfuko wa vijana ili kiwanda hicho kiweze kukua kwa haraka na kuzalisha chaki kwa wingi hivyo kuweza kuzuia soko la chaki zinazotoka nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha chaki Wilayani Maswa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa hadi sasa uzalishaji wa chaki unaofanywa na kiwanda kidogo cha Maswa Youth Family unatosheleza mahitaji ya chaki kwa shule zote za Mkoa huo na kuzipiga marufuku shule zote mkoani hapo kununua chaki nje ya Mkoa wa Simiyu.
“Simiyu imedhamiria kuionyesha nchi kuwa sisi ngozi nyeusi tunaweza tukaibua miradi, tukajenga uwezo na baadaye tukazalisha kwa kuiendeleza kauli mbiu ya mkoa wetu ya bidhaa moja wilaya moja ambayo baadaye itashuka hadi kuwa bidhaa moja kijiji kimoja na kulifanya taifa letu kuwa taifa la viwanda alisema Mhe. Mtaka.
Aidha Naibu Waziri Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Antony Mavunde amesema kuwa Mkoa wa Simiyu umekua wakwanza kuiishi kwa vitendo falsaga ya bidhaa moja wilaya moja na kuahidi kuiunga mkono falsafa hiyo kujitolea kuwa balozi wa Chaki inayotengenezwa na Maswa Youth Family ili kuweza kuitangaza nchi nzima.
Naye Mwenyekiti wa Maswa Youth Family Bw. Kelvin Steven amesema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha chaki 38,400 kwa saa sawa na katoni 16 na iwapo uzailishaji utafanyika kwa saa nne kiwanda kitazalisha katoni 128 kwa siku na uzalishaji huo kwa siku 20 unategemewa kuwa katoni 2560 ambapo mahitaji kwa mwezi kwa Wilaya inakadiriwa kuwa katoni 157 hivyo kuwa na zaidi ya katoni 2403 ambazo zitauzwa maeneo mengine.
Mradi huu umegharimu jumla ya shilingi 37,967,522 kati ya fedha hizo shilingi 30,967,522 ni mchango wa Halmashauri na shilingi 70,000,000 ni mchango wa kikundi uliotokana na fedha za mkopo waliopewa kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Post a Comment