Ads

ALAT NA WABUNGE AFRICA MASHARIKI WAMLLIA MASABURI

Image result for picha za masaburi

 mwambawahabari 
CCM, ALAT, Bunge la Afrika Mashariki wamlilia Masaburi
Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania ( ALAT),  pamoja na Umoja wa Vijana na Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wamesikitishwa na kifo Marehemu Didas Masaburi aliyefariki dunia Oktoba 12, 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika uhai wake Marehemu Masaburi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa ALAT, UVCCM, na Baraza la Wazazi CCM. Pia aliwahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Kati.
Mwenyekiti wa ALAT, Gulam Mukadam ameelezea mchango wa Marehemu Masaburi katika Jumuiya hiyo wakati akiwa mwenyekiti wake, ambapo amesema kuwa alipambana kuhakikisha kwamba mamlaka za  Serikali za Mitaa nchini zinatambuliwa kikatiba.

" Marehemu Masaburi enzi za uhai wake alifanya mengi, leo hii serikali za mitaa zina mamlaka zina uwezo wa kufanya maamuzi yake binafsi na hii yote ni juhudi zake," amesema.
Mbunge wa Mtwara Vijijini Hawa Ghasia, aliyewahi kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amemuelezea Marehemu Masaburi kuwa enzi za uhai wake alipambana kuhakikisha kuwa miundombinu ya jiji la Dar es Salaam hususani ya barabara inajengwa pamoja na kukarabati, kupanua kingo za mito inayosababisha mafuriko.
" Masaburi alianzisha mradi wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, DART lakini na barabara za FIDA ambazo zitakuwa zinaleta wananchi katika barabara za DART na pia katika maeneo ya mito inayosababisha mafuriko makubwa sana, kwa hiyo tuliuanzisha huo mradi na aliusimamia kwa nguvu zote na ninaamini huo mradi ukianza wananchi watamkumbuka Masaburi," amesema.
Naye mwakilishi wa Spika la Bunge la Afrika Mashariki na Kati, Abdallah Mwinyi amesema kuwa Marehemu Masaburi alikuwa mbunge hodari katika bunge hilo kutokana kwamba alikuwa na uwezo wa kujenga hoja zinazohusiana na utetezi wa maendeleo na masilahi ya wananchi wa nchi husika.
Mwenyekiti wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka amemuelezea Masaburi kuwa enzi za utawala wake katika umoja huo alileta mapinduzi ya kiuchumi kwa kuanzisha vitega uchumi vya umoja huo.
"Matunda ya UVCCM tunayoyaona sasa ni kutokana na jitihada za Masaburi, umoja huu hautaweza sahau mchango wake. Alikuwa mshauri wetu baada ya kuachia wadhifa wa uenyekiti. Enzi za utawala wake alifanikisha umoja huu kuwa na vitega uchumi ambavyo tunavitumia hadi sasa," amesema.
Mwili wa Marehemu Masaburi unazikwa leo maeneo ya Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

No comments